Mbio za Mbezi Fun Run zazinduliwa Dar

Muktasari:

Mbio za Mbezi Fun Run zinatarajiwa kushirikisha wakimbiaji wa vikundi mbalimbali (Jogging) vya Dar es Salaam kwa ajili ya kuhamasisha na kutoa hamasa kwa wakazi wa Dar es Salaam kufanya mazoezi.

Dar es Salaam. Mbio mpya za Mbezi Fun Run zimezinduliwa leo Novemba 13, jijini Dar es Salaam zikitarajiwa kufanyika Desemba Mosi.

Mratibu wa Mbio hizo, Omary Kimbau alisema zitashirikisha wakimbiaji wa kilomita 21, 10 na kilomita 5.

Alisema mbio za Mbezi Fun Run zinalenga kuwahamasisha wakazi wa Dar es Salaam kufanya mazoezi, kujenga umoja na kufahamiana.

"Tunamtarajia Waziri wa Afya, Jinsia, Wazee na watoto, Ummy Mwalimu kuwa mgeni rasmi.

Mmoja wa wana kamati wa maandalizi ya mbio hizo, Christina Manogi (Sinta), alisema mbali na mbio siku hiyo pia watafanya usafi katika eneo la wazi la fukwe lililo jirani na hoteli ya Ramada Mbezi, ambako mbio zitaanzia.

Alisema pia siku hiyo wakimbiaji watashiriki kuchangia damu na kupima ukimwi kwa hiari.

Mwenyekiti wa mbio hizo, Rolaa Robelo alisema fomu za kushiriki zitaanza kutolewa Ijumaa hii kwenye maeneo mbalimbali jijini Dar es Salaam.