Simba wapewa ishu za kuiua mapema Mbambane

Muktasari:

Simba imepewa ushauri wa bure kuelekea mechi yake ya Ligi ya Mabingwa Afrika, inayotarajia kuanza kati ya 28 na 29, kuhakikisha wanatumia muda uliobaki kuwajenga wachezaji wao kiakili.

Dar es Salaam.Kocha wa timu ya vijana ya Azam, meja mstaafu, Abdul Mingange amelishauri benchi la Simba pamoja na viongozi kuwajenga kiakili wachezaji wao kabla ya mchezo wa Ligi ya Mabingwa dhidi ya Mbambane Swallows.

Mingange alisema kocha mkuu wa Simba, Patrick Aussems aendelee kusaka mbinu za ufundi hasa akiwa anapiga jicho na upande wa pili kujua wana kikosi gani, kisha awe anawaaminisha wachezaji wake waendane na uhalisia wa wapinzani wao.

"Unajua akili ikiwa tayari inafanya hata mwili uitikie kufanya kazi, ndio maana mwanafunzi asipomwelewa mwalimu anafeli ndivyo ilivyo kwa mchezaji, lazima umjenge kiakili kutambua anachokwenda kukifanya, Simba ni timu nzuri waondoe papara na kuona wanakutana na timu ya maajabu.

"Mbambane Swallows inafungika, wajiamini lakini huku wakiwa na tahadhari ya nidhamu ya hali ya juu kwa maana kutumia vyema nafasi wanazozipata, kila mchezaji kusimama kwenye majukumu yake akijua anapofanya hafifu anakwamisha mipango ya timu,"anasema.

Mbali na hilo pia ameizungumzia Mtibwa Sugar, kujua ukubwa wa michuano hiyo na kudai kwamba Watanzania wanawategemea wafike mbali "Nazungumza kiufundi, ndani ya kikosi cha Mtibwa Sugar hakina wachezaji wengi wazoefu na michuano hiyo,"anasema.