Ugumu wa Ligi Kuu wamtisha Liuzio

Monday November 12 2018

 

By SADDAM SADICK

Mwanza. Mshambuliaji wa Mtibwa Sugar, Juma Liuzio amekiri Ligi Kuu msimu huu ni mgumu kwao, huku akifafanua kuwa bado wanaamini watafanya vziuri hata kimataifa kutokana na morali waliyonayo.

Mtibwa Sugar wapo nafasi ya nne kwenye msimamo wa Ligi Kuu Bara, ambapo imevuna pointi 23, huku ikiwa imeshinda michezo mitano, sare mbili na kupoteza mechi tano.

Liuzio alisema katika mipango yao walihitaji kushinda mechi zote ili kumaliza mzunguko wa kwanza wakiwa kileleni lakini mambo yameenda tofauti.

Alisema kuwa licha ya ugumu na ushindani kwenye michuano hiyo, wanaamini watabadilika na kufanya vizuri ikiwamo mashindano ya Kombe la Shirikisho Afrika.

“Kwa ujumla ligi ni ngumu kwa sababu mipango yetu ilikuwa ni kushinda mechi zote na kumaliza mzunguko wa kwanza tukiwa kileleni ila imekuwa tofauti, bado tunaweza kufanya vizuri kutokana na morari tuliyonayo hata kimataifa”alisema nyota huyo.

Mshambuliaji huyo wa zamani wa Simba alisema idadi ndogo ya mabao aliyofunga yanatokana na kukosa bahati kwani licha ya kutengeneza nafasi nyingi, lakini ameshindwa kufunga mabao.

Alisema mabeki wamekuwa wakikamia jambo ambalo limempa ugumu, na kuahidi mashabiki wake watulie kwani Ligi itakapoendelea atakuja na mbinu mpya kuhakikisha anafanya kweli.

“Ni kukosa bahati tu, lakini nafasi nazipata za kufunga mabao, ila mabeki nao wananikamia, matarajio yangu nitafunga sana kwahiyo mashabiki wangu watulie nitarudi na mbinu mpya”alisema Straika huyo.

Advertisement