Mbunge Chumi: Ukata utaua soka la Tanzania

Muktasari:

Mbunge ahofia soka la Tanzania kupolomoka kutokana na klabu kukosa fedha za kumudu gharama za kujiendesha katika msimu huu wa Ligi Kuu Bara.

Dodoma. Mbunge wa Mafinga, Cosato Chumi amesema bila serikali kuingilia kati, soka la Tanzania linaelekea kufa.

Chumi ametoa kauli hiyo bungeni leo Novemba 12, 2018 alipoomba mwongozo wa spika akitaka ufafanuzi wa namna ya kulisaidia Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) ili kuunusuru mpira wa Tanzania.

Mbunge huyo amesema bila serikali kuingilia kati na kutafuta mfadhiri, kuna baadhi ya klabu kubwa nchini zinaweza kujikuta zikishindwa kushiriki mashindano.

"Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba mwongozo wako, ni vipi Serikali inaweza kuisaidia TFF kupata mfadhiri kwani baadhi ya klabu ziko hoi na bila kuingilia katika watashindwa hata kuendelea na ligi hiyo."

Katika Kujenga hoja mbunge huyo amesema soka ndiyo kila kitu kwani inasaidia kuingiza fedha, ni ajira kwa vijana na inaweza kuwa fursa nzuri kwa jamii.

Mwenyekiti wa bunge Andrew Chenge amesema mwongozo huo asingeutolea ufafanuzi kwani jambo hilo halikutokea mapema bungeni.

Hata hivyo Chenge aliitaka Serikali kuchukua hoja za mbunge huyo na kuzifanyia kazi kwa tahadhari ili kunusu soka la Tanzania.