Eti! Nduda wa Simba anaijua Mbambane Swallows

Saturday November 10 2018

 

By OLIPA ASSA

Dar es Salaam. Licha ya kipa wa Simba, Said Mohammed 'Nduda' kukosa nafasi ya kucheza mbele ya Aishi Manula na Deogratius Munishi 'Dida' hakujamfanya ashindwe kuifuatilia Mbambane Swallows watakaofungua nao katika mashindano ya Ligi ya Mabingwa Afrika.

Nduda amesema akiwa mmoja wa wachezaji wa kikosi hicho cha Simba, inamlazimu kujua  kila kitu kinachoihusu timu yake na si kulaumu kwa nini anakosa nafasi.

"Naingia kwenye mitandao ya kijamii na kuangalia ina wachezaji wa aina gani wapi wazuri na wabaya, suala la kuwa ninacheza au sichezi hilo ni lingine. Ikitokea nikapangwa nicheze nitafanyaje kama si kuumbuka,"alisema Nduda aliyewahi kuzichezea timu za Yanga na Mtibwa Sugar.

"Mchezaji makini ni yule anayepambana na changamoto bila kujali alivyoshindwa leo, anakuwa anaipambania kesho yake itakuwa vipi, ndicho ninachokiishi, najituma mwanzo mwisho bila kujali kupata nafasi mbele ya makipa wenzangu na kikubwa najiamini nina uwezo."

Tangu ajiunge na Simba msimu uliopita akitokea Mtibwa Sugar, Nduda alibahatika kucheza mechi mbili tu na tangu msimu mpya uanze sasa ikiwa ni mzunguko wa 14, bado hajapata nafasi na kocha mkuu wa timu hiyo, Patrick Aussems anamchezesha Aishi Manula.

Advertisement