Pluijm: Chirwa ni mtovu wa nidhamu?

Muktasari:

Sababu zinazodaiwa kuwa Chirwa alionyesha utovu wa nidhamu ndani ya kikosi cha Yanga ni baada ya kujiweka pembeni katika baadhi ya mechi akigoma kucheza kwa sababu ya maslahi na baadaye aliamua kuondoka kabisa.

Dar es Salaam. Kocha Mkuu wa Azam FC, Mholanzi Hans Pluijm amesema wanaosema Mzambia Obrey Chirwa ni mtovu wa nidhamu wataona atakavyofanya naye kazi.

Pluijm amesema, kama mchezaji huyo ni mtovu wa nidhamu mbona alifanya kazi nzuri na yeye vizuri ndani ya kikosi cha Yanga.

"Hizo ni stori tu inabidi kujiuliza mbona nimemfundisha Chirwa na sikuwa na tatizo naye,"alisema Pluijm ambaye ana uzoefu na wachezaji pamoja na mpira wa Afrika baada ya kufundisha klabu mbalimbali kama Yanga, Singida United na sasa Azam.

Amefafanua, wakati anavunja mkataba wake na Klabu ya Nogoom El Mostakbal Football Club aliwasiliana naye na hamu yake ilikuwa aende Azam.

Lakini, kwa sababu yeye pia ndani ya Azam ana wakubwa wake lazima wajadiliane na kukubaliana juu ya ujio wake.

Awali, Chirwa aliichezea Yanga akitokea Platinumz FC ya Zimbabwe lakini aliondoka na kwenda Misri ambako alijiunga na klabu hiyo ya Nogoom ya Misri.

Akiwa huko mambo hayakwenda sawa na Chirwa aliamua kuvunja mkataba na kurudi Tanzania sababu ikiwa ni tofauti katika maslahi.