Gauni la harusi mke wa Tambwe acha kabisa!

Saturday November 10 2018

 

By DORIS MALIYAGA

Dar es Salaam.LICHA ya ubabe wake wa kuzifumania nyavu, straika Mrundi, Amisi Tambwe amenasa kwenye penzi nzito la mrembo wa Kitanzania, Raiyan Mohammed ambaye juzi Alhamisi usiku walifunga pingu za maisha.
Tambwe ambaye anatamba kwenye Ligi Kuu Bara kutoka na ubora huo alipotua Simba akitokea Vital 'O' ya Burundi na baadaye Yanga anayoichezea mpaka sasa, amefunga ndoa na rembo huyo mzaliwa na Mbeya lakini asili yake ni Uarabuni.
Kila kitu kilifanyika huko Buguruni Lozana na usiku wa leo Jumamosi maeneo ya Ilala Bungoni, kutakuwa na sherehe nyingine kabambe ya usiku wa zawadi.  
Sherehe hizo tofauti zinazohudhuriwa na mastaa tofauti ilianza na Singo maeneo ya Kariakoo ambapo Raiyan alifurahi na wanawake wenzake kwa kumpamba na zawadi. Katika sherehe hiyo ya Singo ambayo ni kama Kitchen Part sehemu kubwa ya wanawake waliofika ni wake wa wachezaji ambapo alikuwepo mke wa Kelvin Yondani 'Vidic' anayeitwa Nance Mussa, wa Ibrahim Ajibu (Amina) na wa Geofrey Taita (Ashama Mabrouk).
Siku hiyo walifika wachezaji wenzake wa Yanga akiwemo, Juma Abdul pamoja na viongozi wake, Kaimu Katibu Omary Kaaya, Mratibu Hafidh Salehe na Meneja Nadir Haroub 'Cannavaro'.  
Lakini, baada ya matukio yote matatu, la nne litakuwa ni lile kubwa litakalofanyika nchini Burundi nyumbani kwa kina Tambwe kwa ajili ya kuwapongeza wawili hao na itakuwa baada ya mzunguko wa kwanza Ligi Kuu kumalizika.

GAUNI BIBI HARUSI
Katika sherehe hizo, mpango mzima ni namna bibi harusi huyo anavyovaa ndani ya siku hizo tatu. Raiyan anaweka wazi bei ya magauni matatu pamoja na viatu.
"Sipendi mambo makubwa, nitavaa nguo zenye gharama ya kawaida ambapo, gauni la singo (Kitchen Part) ni la rangi ya pinki, nimelinunua Sh300,000, la ndoa ni rangi ya pichi Sh200,000 na la usiku wa zawadi ni Sh500,000,"anasema Raiyan ambaye ni shabiki wa Manchester United na anavutiwa zaidi na soka la Cristiano Ronaldo ingawa baada ya kuondoka amegeukia kwa Marcus Rashford.
"Gharama ya viatu vya matukio yote matatu kila kimoja nimenunu kwa Sh30,000 na kufanya jumla ya Sh 90,000."
Anafafanua kuwa lengo la kununua na si kuvaa ya kukodi, ni baada ya kuona gharama zake hazitofautini kwa kiwango kikubwa.

TAMBWE HASUMBUI
Katika maisha ya mume na mke ndani ya nyumba kupishana kauli ni kawaida na Raiyan analiunga mkono hilo lakini ukweli wa undani wao ni huu.
"Changamoto za maisha ndani ya nyumba huwa hazikosani lakini nasema ukweli, najivunia kuwa na Tambwe kwa sababu ni mwanaume wa aina yake na katika maisha yetu hajawahi kuniweka katika kipindi chochote kigumu. Ni mwelewa, ana upendo na anajali sijawahi kujuta,"anasema Raiyan ambaye anaishi na Tambwe nyumba moja kwa kipindi cha takribani miaka minne.
Anafafanua kuwa wachezaji wana sifa ambazo wakati mwingine si nzuri, kwa Tambwe iko hivi "Tambwe hayupo hivyo na si kila mchezaji yuko na tabia za ajabu."

TAMBWE NI CHAI NA CHAPATI
Baadhi ya wachezaji wengi wanaaminika kuwa mambo ya msosi kwao si mchezo kwani wanapoamua kula ni balaa. Raiyan anasema, chakula cha Tambwe ni kawaida na kuna wakati huwa hali kabisa.
"Anapoamka Asubuhi kama hana ratiba ya mazoezi huwa ni saa nne hivi. Baada ya hapo anakunywa chai na mara nyingi huwa na kitafunwa cha chapati, mchana ni ugali mboga za kawaida kama ni nyama, samaki, majani na matunda na usiku ni wali na mboga za hivyo,"anasema.
"Anakula kawaida na huwezi kuamini, siku anayocheza mechi usiku huwa hali kabisa chakula zaidi ya kunywa vitu kama juisi na maji."
Anafafanua, Tambwe si mtu wa kuzurura, kama hayuko kambini atakuwa nyumbani anaangalia 'movie' na ukifika muda wa chakula atakula na kulala.
"Jioni anapenda kwenda gym kwa ajili ya mazoezi na anapomaliza huwa ni nyumbani tu,"anaeleza.

BAADA YA KUSTAAFU WATAISHI WAPI?
Raiyan anafafanua kuwa baada ya maisha ya mpira ya Tambwe hapa Tanzania, makazi yao yatakuwa Burundi ambako ni nyumbani kwa kina Tambwe.
"Kule ndiyo kuna maisha yote na nyumba imejengwa huko labda hapo baadaye mambo yatakapokuwa mazuri tunaweza kuongeza nyingine hapa Tanzania,"alifafanua.

HANA MPANGO NA MAGARI YA FAHARI
Ukimtazama Raiyan kuanzia kichwani hadi mguuni ni mrembo na kwa haraka unaweza kusema mwanamke huyo ni wa gaharama au ni mpenda makuu na lakini utakachokisoma ndiyo ukweli juu maisha yake.
Raiyan ni mwanamke wa kawaida tofauti kabisa na wale wenye kupenda maisha ya kifahari. Licha ya kuwa Tambwe anamikili gari aina ya Toyota Land Cruiser ya kisasa, yeye hana hata mpango nayo.
"Tambwe anapokuwa kazini, gari inakuwa tu nyumbani lakini katika safari zangu natumia boda, bajaji na taxi tu, natumia Land Cruiser ninapokuwa na Tambwe mwenyewe pale tunapoamua kutoka pamoja,"alisema Raiyan ambaye anakiri mpaka sasa hata leseni ya udereva hana.
"Si kama ananikataza, binafsi sipendi tu mambo makubwa kwa sababu hata usafiri huu nafanya mambo tena kwa haraka zaidi."
Anasema, yeye mtu wa kawaida katika maisha yake, hana dharau na anaheshimu kila mtu mdogo kwa mkubwa.

KINACHOMKERA
"Kitu ambacho Tambwe hakipendi Tambwe ni kukuona unazurura hovyo, hutulii nyumbani. Anapenda muda wote uwe nyumbani na unapotoka iwe kwa mambo muhimu na hiyo ndiyo furaha yake,"anaeleza Raiyan ambaye anaweka wazi kuwa yeye ni shabiki wa Mbeya City lakini kwa sababu Tambwe anacheza Yanga, anamuunga mkono mumewe.
Anafafanua namna, Tambwe alivyo: "Ni mtu wa kawaida kwa namna alivyo, unaweza kusema ni wa namna gani kwa sababu maisha yake ni ya kawaida mno."

KILICHOMSHUSHA KIWANGO TAMBWE
Katika siku za karibuni kiwango cha Tambwe ni kama kimeshuka kwa sababu ni tofauti na ilivyokuwa awali na Raiyan anafafanua.
"Majeruhi ndiyo sababu kubwa jambo linalosababisha ichukue muda mrefu kurudi katika kiwango chake. Inaniuma lakini sina jinsi na ninachoamini atarudi tu katika kiwango chake cha kawaida,"anasema Raiyan.
Amezungumzia inavyokuwa baada ya mechi na kurudi nyumbani iwe wameshinda au wamefungwa anakuwa na majukumu ya familia "Ya uwanjani huwa anayaacha huko na nyumbani ni familia tu."

HISTORIA YA NDOA
Ni miaka mitano imepita tangu Raiyan na Tambwe wakutane pale maeneo ya Ilala, Boma. Ilivyokuwa, Tambwe alimpa lifti Raiyan kwenda mjini na hapo ndipo walibadilishana namba za simu wakaanza kuwasiliana na baadaye kuwa wapenzi.
"Sikuwa na mazoea na Tambwe lakini nilijua ni mchezaji. Tulipokuwa pamoja nilipoona tunaendana ikabidi iwe hivyo hadi sasa miaka inapita,"anasema Raiyan.
Anasema, wakiwa kwenye mahusiano wamefanikiwa kuzaa mtoto mmoja anaitwa Ayman mwenye mwaka mmoja, lakini, Tambwe anaye mwingine mkubwa aliyemzaa Burundi.

Advertisement