Ndemla aizamisha Azam

Saturday November 10 2018

 

By THOBIAS SEBASTIAN

Dar es Salaam.MABINGWA watetezi wa Ligi Kuu Bara Simba jana Ijumaa waliendelea kujifua, bila ya nyota wao kadhaa lakini bao la Said Ndemla lilitosha kuizimisha timu ya vijana ya Azam U20.
Ndemla alifunga bao hilo kipindi cha kwanza kwenye Uwanja wa Gymkhana huku Kocha Mkuu wa Azam, Hans Pluijm na Meneja wa vinara hao wa Ligi Kuu Bara, Philip Alando na beki Yakub Mohammed wakishuhudia.
Mara baada ya kumalizika kocha wa Simba, Patricks Aussems ambaye aliondoka na ushindi alisema kwake hiyo haikuwa mechi bali ni mazoezi na alitaka kuona vijana wake wanacheza kwa kupasiana pasi nyingi dakika zote tisini.
“Kwangu haikuwa mechi ilikuwa ni sehemu ya mazoezi kwa maana hiyo sina zaidi la kuongea ila niwapongeze vijana wa Azam wamecheza kwa kujiamini,” alisema.
Naye Kocha wa Azam U20, Meja Mstaafu Abdul Mingange alisema akili yao ya kwanza walifahamu kwamba hawataweza kuwafunga Simba ila aliwambia vijana wake wacheze mpira kwa muda mrefu ndio wataweza kuwazuia.
Hans Pluijm naye alisema vijana wamecheza vizuri na wanajiamini ni wazi kwamba wakiendelea kupata nafasi ya kucheza mechi kubwa na za ushindani kuna ambao atawapa nafasi katika timu kubwa na wengine kupata timu za madaraja ya juu.
“Mara ya mwisho tunacheza nao walitufunga mabao 3-2 na kwa walivyocheza mechi hii na Simba tusipokuwa makini wanaweza kutufunga tena katika mechi ijayo kwani wanaonekana kuimarika zaidi ya awali.”

Advertisement