Okwi, Kagere hapa tu freshi tu Nyoni, Wawa wanakazi

Saturday November 10 2018

 

By Charles Abel, Thobias Sebastian, Olipa Assa na Mwanahiba Richard

Dar es Salaam. MASTRAIKA wa Simba, Meddie Kagere, Emmanuel Okwi, John Bocco na Adam Salamba wakijipanga freshi huenda wakawapa raha mashabiki wao kwani kwa sasa wana kazi moja tu ya kutupia ili kuing'oa Mbabane Swallows ya Eswatini.
Simba itakayoshiriki Ligi ya Mabingwa Afrika, imepangwa kuanza mechi ya raundi ya awali dhidi ya wababe hao wa Eswatini (Swaziland) baada ya Shirikisho la Soka Afrika (CAF) jana kuanika ratiba nzima pamoja na ile ya Kombe la Shirikisho Afrika.
Mechi hizo za awali ambapo Simba itaanzia nyumbani, zitachezwa kati ya Novemba 27-28 kabla ya kurudiana wiki moja baadaye ambapo kama Mnyama atapenya hatua hiyo atavaana ama Nkana ya Zambia  anayoichezea beki wa kimataifa wa Tanzania, Hassan Kessy ama UD Songo ya Msumbiji.
Hata hivyo tayari baadhi ya mashabiki washaanza kuhisi kama Simba imepata mchekea, ila ukweli Mbabane sio timu nyepesi na lazima nyota wa Simba hasa kina Kagere, Okwi na Bocco wafanye yao nyumbani na ugenini mambo yawe poa.
Mastraika hao watakuwa na kazi na kuupita ukuta wa wapinzani wao utakaokuwa chini ya mabeki wenye roho mbaya wakiongozwa na Mandla Palma, Mhlonipheni Matsebula, Ndaba Joseph Ndumiso, Sanele Justice Mkhweli, Siboniso Nkhosinathi Ndzabandzaba, Sifiso Lucky Mabila na Sizolwethu Shabalala.
Mabeki hao wakisaidiana na viungo matata wa klabu hiyo wameisaidia Mbabane mpaka sasa kucheza mechi 9 na kushinda tano wakitopka droo mbili na kupoteza mbili, huku wakiruhusu mabao nane na wenyewe wakifunga mabao 11.
Kwa kasi ya kina Kagere na Okwi ambao wana mabao saba kila mmoja mpaka sasa katika Ligi Kuu Bara wakisaidia na kina Bocco na Salamba wenye mabao mawili kila mmoja, kama wakijiamua kukoma Simba itavuka hapo salama.
Kwani ni wazi, timu hiyo inafungika kirahisi, licha ya mabeki wake kuonekana hawana mchezo katika mechi wakivaana na timu yenye washambuliaji wasumbufu.
Mbali na kazi waliyonayo kina Kagere atakayeichezea Simba kwa mara ya kwanza michuano ya CAF, pia mabeki wa Simba watakuwa na kazi ya kuwachunga nyota wa Mbabane ambao wanafunga mabao yao kupitia viungo.
Banele Sikhondze na  Felix Gerson Badenhorst ndio tishio zaidi kwani Felix katika mechi ya makundi ya Ligi ya Mabingwa  mwaka huu amefunga mabao manne kazi inayofamya mabeki Pascal Wawa, Erasto Nyoni na kina Shomary Kapombe na kipa Aishi Manula kujipanga kwelijkweli.
Mbali na viungo, Mbabane ailiwang'oa Azam mwaka jana katika michuano ya Shirikisho, inawastambuliaji hatari wakiongozwa na Mghana Daniel Arakora, Jean Claude Amougou na wengine ambao wanajua sana kutupia.

MBELGIJI FRESHI
Kocha Mkuu wa Simba, Patrick Aussems alisema kwa kifupi juu ya droo hiyo ya CAF; akisema kwake haina tatizo.
“Kwangu naweza kusema droo imefanyika vizuri na inaweza kuwa nzuri kwetu kama tutapata nafasi ya kufuzu kwenda katika hatua ya mbele zaidi,” alisema kabla ya kuongeza;
“Inaweza kuwa droo mbaya kwetu kama tutashindwa kufuzu katika hatua ya mbele zaidi ya mashindano haya kwani malengo yetu msimu huu ni kufanya na nitaongeza nguvu zaidi ya kuwafuatilia wapinzani ili kufahamu mambo yao."

WADAU WAFUNGUKA
Wadau mbalimbali wa soka walitoa maoni yao juu ya droo hiyo kwa Simba na hata wawakilishi wengine wa Tanzania wakiwamo Mtibwa Sugar ambapo Mussa Hassan Mgosi alisema;
“Mashindano haya ni klabu bingwa kwa maana hiyo kila timu ilikuwa bingwa katika ligi ya kwao hakuna timu ambayo itakuwa dhaifu katika mashidano haya ambayo yanataka pia matumizi mazuri ya mechi za nyumbani,” alisema.
“Simba ina kikosi kizuri katika kila nafasi kuna zaidi ya wachezaji wawili wenye uwezo sawa kwahiyo jukumu hilo limebaki kwa kocha kujua na kuwatambua wapinzani ili kuweza kupata matokeo mazuri katika mechi zote mbili,” alisema.
Upande wa Ally Mayay alisema; “Simba kwanza wanatakiwa kutumia uwanja wa nyumbani kupata ushindi wa mabao mengi maana timu ya kwetu hapa Tanzania huwa hazina uwezo wa kwenda kushinda katika mechi za ugenini kwa maana ya kupindua matokeo kama nyumbani watakuwa wamefanya vibaya.”
Kocha msomi Dk Mshindo Msola alizungumzia ratiba ya michuano ya kimataifa  inayowakabili Simba ambao pia wataanzia nyumbani dhidi ya Mbambane Swallows alisema ni lazima Simba wawe makini.
"Ubora wa Simba unaonekana kwenye timu ambazo hazina nguvu kiuchumi na ligi yetu mbovu, wamesajili vizuri na kikosi kipana ila si kwa kujiamini kwa asilimia kubwa michuano ya kimataifa, Mbambane Swallows siyo timu ya kuidharau wanapaswa wajiandae vyema kwani hawajui silaha za wapinzani wao, Watanzania pia wajiandae kwa lolote kwenye matokeo wakidharau basi safari inaweza kuwa ngumu kwao.

MBABANE WATAMU
Mbabane Swallows iliyoasisiwa mwaka 1948 ni miongoni mwa timu chache kutoka Kusini mwa Bara la Afrika ambazo katika miaka ya hivi karibuni imekuwa ikifanya vyema kwenye mashindano ya kimataifa.
Katika kipindi cha miaka mitano iliyopita, Swallows wameshiriki mashindano ya CAF mara zote kulinganisha na Simba ambayo kuanzia 2013 hadi sasa imeshiriki mara mbili tu na kutolewa hatua za mapema.
Mabingwa hao wa Eswatini, wana rekodi nzuri kwa kufuzu mara mbili mfululizo hatua ya makundi ya mashindano ya Afrika kwa klabu jambo linalowapa uzoefu zaidi.
Mwaka 2017 walifanikiwa kufuzu  makundi ya Kombe la Shirikisho kwa kuzitoa timu za Orapa United, Azam FC na AC Léopards kwenye hatua za mtoano lakini walimaliza wakiwa nafasi ya tatu kwenye kundi B nyuma ya timu za CS Sfaxien, MC Alger wakati timu ya Platinum Stars ilishika mkia.
Katika hatua hiyo Swallows walimaliza wakiwa na pointi tano baada ya kuibuka na ushindi kwenye mechi moja, kutoka sare mbili na kuchapwa mechi tatu.
Kuonyesha kwamba hawakubahatisha kuingia hatua hiyo msimu mmoja nyuma yake, mwaka huu tena walifuzu hatua ya makundi kwenye Ligi ya Mabingwa Afrika baada ya kuzitoa timu za Bantu na Zanaco kwenye hatua ya mtoano.
Ilikuja kukwama kwenye hatua ya makundi mbele ya timu za Etoile Du Sahel, De Agosto na Zesco United baada ya kushika nafasi ya mwisho ikishinda mchezo mmoja na kutoka sare moja huku mechi zilizobakia nne ikipoteza.
Iwapo Simba ikifanikiwa kuitoa Mbabane Swallows, inaweza kujikuta ikiangukia kwa kigongo kingine, timu ya UD Songo ya Msumbiji ikiwa nayo itaweza kuitoa Nkana Red Devils ya Zambia.
UD Songo kama ilivyo kwa Swallows, nayo imekuwa ikifanya vizuri kwenye mashindano ya Afrika katika miaka ya hivi karibuni.
Mwaka huu timu hiyo ya Msumbiji ilifika hatua ya makundi ya Kombe la Shirikisho Afrika ambako iliishia nafasi ya 3 kwenye kundi B ikiwa na pointi tatu, ikifunga mabao matano na kufungwa kumi.

MTIBWA NAO
Mtibwa Sugar imebahatika kuanza mchezo wake wa kwanza wa Kombe la Shirikisho Afrika nyumbani kwa kuwapokea Northern Dynamo ya Shelisheli, mechi itakayopigwa kati ya Novemba 27 na 29.
Jambo ambalo kocha mkuu wa Mtibwa Sugar, Zuber Katwila ni kama alikuwa anasubiria kwa hamu ratiba ya michuano hiyo ipangwe kwani baada ya kujua watacheza na Northern Dynamo ya Shelisheli, alisema wapo tayari kwa kazi.
"Tulijiandaa muda mrefu kwani saikolojia zetu zinajua tuna jukumu zito la michuano ya kimataifa mwaka huu, kikosi chetu kitakuwa kile kile ikitokea tukasajili basi ni mchezaji wetu achukuliwe na timu pinzani," alisema Katwila.
Alipoulizwa kama watacheza mechi ya kirafiki ya kimataifa kama maandalizi dhidi ya Northern Dynamo ya Shelisheli! Katwila alijibu kwa kicheko kuwa "Kwetu tukicheza mechi za ligi dhidi ya Simba na Yanga tutakuwa tumejipima vya kutosha maana ndio za kimataifa,"alisema.
Dk Msolla alisema; "Mtibwa Sugar nao wanapaswa kujipanga kujua Watanzania wanahitaji kuona wanasonga mbele kwenye michuano hiyo, kikubwa wajue wapinzani wao wana ligi bora na wana viwango bora uwanjani."
Straika wa zamani wa Simba, Dua Said aliwataka viongozi wa timu hiyo kwenda kufanya uchunguzi kwa wapinzani wao Mbambane Swallows kabla ya kukutana kwenye mechi, ili kujua wana ubora gani na mapungufu yao.
"Kuwachunguza wapinzani mapema ndio jambo la msingi, wakiwajua ni wa aina gani ndipo Aussems anaweza kubadili mfumo wake utakaoendana na uhalisia wa mechi anayocheza," alisema.

Advertisement