Kikosi kizito cha Mtibwa Sugar Kombe la Shirikisho moto uleule

Friday November 9 2018

 

By Saddam Sadick

Mwanza. Licha ya kudai safu ya ulinzi kufanya makosa katika mchezo wa Ligi Kuu Tanzania Bara dhidi ya Alliance, Kocha wa Mtibwa Sugar Zuberi Katwila amesema hatapangua kikosi.

Akizungumza jana, Katwila alisema hana mpango wa kupangua kikosi kwa kuwa ana wachezaji wenye viwango bora wanaoweza kushindana katika mashindano yote yanayoikabili Mtibwa Sugar.

Kauli ya Mtibwa Sugar imekuja muda mfupi baada ya timu hiyo kucharazwa bao 1-0 kwenye Uwanja wa CCM Kirumba, Mwanza.

Katwila alisema kuwa mabeki walizembea kuokoa hatari langoni hatua iliyochangia Alliance kupata bao ambalo liliizamisha Mtibwa Sugar.

Kocha huyo alisema ingawa Mtibwa Sugar inajiandaa kwa mashindano ya Kombe la Shirikisho, hana mpango wa kusajili mchezaji katika dirisha dogo la usajili lililopangwa kufunguliwa Novemba 15 hadi Desemba 15.

“Sina mpango wa kuongeza mchezaji kwa sababu kikosi changu kina vijana mchanganyiko niliopandisha kutoka timu ya vijana,”alisema Katwila.

Mchezaji huyo wa zamani wa timu hiyo, alisema uzembe wa mabeki waliofanya dhidi ya Alliance, hauwezi kumtoa katika mpango wake wa maandalizi ya kujiandaa na mashindano ya kimataifa.

Alisema ana amini Mtibwa Sugar ina wachezaji hodari wanaoweza kushindana katika Ligi Kuu na kipigo dhidi ya Alliance ni sehemu ya mchezo.

Mtibwa Sugar yenye maskani Manungu, Morogoro imevuna pointi 13, inashika nafasi ya nne katika msimamo wa Ligi Kuu nyuma ya Azam, Simba na Yanga.

 

Advertisement