FKF yaipigia magoti serikali, yaomba milioni 83

Muktasari:

Hii sio mara ya kwanza kwa FKF kuikimbilia serikali kwani kuomba msaada, kwani itakumbukwa kuwa majumaa mawili yaliyopita, Mwendwa alizungumza a waandishi wa habari ofisini kwake na kusisitiza kuwa ipo haja ya serikali kuingilia kati swala la ukata unaowakabili.

Nairobi, Kenya. Timu zote za taifa zipo katika hali ngumu ya kiuchumi. Harambee Stars, Harambee Starlets na wadogo zao Emerging Stars, wote wapo hoi na sasa kwa mara nyingine tena, Shirikisho la Soka nchini (FKF), limeiangukia Serikali, ikiomba msaada kabla mambo hayajaharibika.
Ni kwamba, timu zote tatu, zinajiandaa kuwakilisha nchi katika michuano ya mikubwa ya bara hili na ili kufanya hivyo, zinahitajika jumla ya shilingi 83 milioni, vinginevyo Kenya inaweza kusahau ushiriki wake kwa sasa.
Kwa mujibu wa Rais wa FKF, Nick Mwendwa ni kwamba, Harambee Stars, inayojiandaa na mechi ya Novemba 18, Ugani Moi Kasarani, kusaka tiketi ya kufuzu kombe ya mataifa ya Afrika (AFCON 2019), dhidi ya Sierra Leone, Ugani Moi Kasarani, inahitaji shilingi 18 milioni.
Kikosi cha wanawake, Harambee Starlets, ambayo itaondoka nchini Novemba 14, kuelekea Accra Ghana, kushiriki michuno ya AWCON, ikiwa ni mara ya pili mfululizo, inahitaji shilingi 43 milioni kugharamia uwepo wao nchini Ghana kuanzia Novemba 14 hadi Desemba mosi, mwaka huu.
Kwa upande wao, kikosi cha U23, maarufu kama Emerging Stars, ambao wanajiandaa kukipiga na Mauritius, Novemba 14, mwaka huu, kusaka tiketi ya kwenda fainali za AFCON U23, zitakazofanyika mwakani nchini Misri, wanahitajikihitaji shilingi 23 milioni.
Kutokana na hilo, Mwendwa alisema, kuna hatari ya Kenya kujitoa kwenye mechi zote hizo, kama hawatopata fedha huku akisisitiza kuwa ni lazima kiasi cha shilingi 43 milioni kipatikane kabla ya Jumanne ya wiki ijayo, la sivyo Starlets, wataisahau AWCON.
“Tutakuwa na timu tamu kambini, Stars, Starlets na Emerging Stars, ukiangalia gharama za uendeshaji wa kila siku, utagundua kuna mzigo mkubwa sana. hivi sasa sisi hatuna fedha, tumeiandikia Serikali kuhusu ombi la kupewa milioni 83, lakini mpaka sasa kimya,” alisema Mwendwa.
Hii sio mara ya kwanza kwa FKF kuikimbilia serikali kwani kuomba msaada, kwani itakumbukwa kuwa majumaa mawili yaliyopita, Mwendwa alizungumza a waandishi wa habari ofisini kwake na kusisitiza kuwa ipo haja ya serikali kuingilia kati swala la ukata unaowakabili.
 “Mpaka sasa hatujajibiwa na serikali, tunafahamu kuwa kuna kiasi cha bilioni 12, zilizotengwa kwenye mfuko wa michezo. Tunafahamu kuwa bunge imeiagiza serikali kutupatia fedha kutoka katika mfuko huo, lakini kama tutazidi kujivuta, huenda tukashindwa kusafiri timu,” alimalizia Mwendwa.