Madogo wa Everton wairarua Gor Mahia 4-0

Muktasari:

Mchezo wa jana usiku ugani Goodison, licha ya kuisha kwa kipigo kizito cha 4-0 kutoka kwa wenyeji wao Everton, uliifanya Gor Mahia kuwa klabu ya kwanza kutoka Afrika Mashariki, kuwahi kucheza na klabu ya EPL, katika ardhi yao.

Nairobi, Kenya. Licha ya kupangiwa kikosi cha watoto watupu katika mchezo wa jana usiku wa kihistoria uliopigwa ugani Goodison Park, mabingwa wa ligi kuu ya Kenya (KPL), waliopanga ‘full’ kikosi, walishindwa kutamba dhidi ya Everton FC.
Mabao 4-0, yalitosha kabisa kuwazima mabingwa hao mara mbili wa kombe la SportPesa, waliosafiri hadi Uingereza kwa lengo la kujaribu kulipiza kisasi dhidi ya Everton ambao waliwafunga 2-1 walipokuja Afrika mwaka jana.
Mabao mawili kutoka kwa Broadhead Nathan na Oumar Niasse, ambao waliingia katika kipindi cha pili wakitokea benchi, yaliwazika kabisa vijana wa Dylan Kerr ambao walijikuta wakipoteza mwelekeo katika dakika ya 16, kipindi kwanza na kumruhusu Ademola Lookman afunge bao la kuongoza.
Dakika saba baadae, muuaji yule yule aliyewamaliza walipokutana Jijini Dar es salaam, mwaka mmoja uliopita, Kieren Dowell, alifanya yake na kumuacha kipa wa Gor Mahia, Boniface Oluoch akiwa hana la kufanya. Hadi mapumziko Everton, walikuwa mbele 2-0.
Kilikuwa ni kipigo cha mbwa mwizi, lakini fursa kubwa kwa mabingwa hao 17 wa KPL, ambao wameweka historia ya kuwa klabu ya kwanza kutoka Afrika Mashariki, kuwahi kucheza na klabu ya ligi kuu ya Englanda (EPL), katika ardhi yao.