Tuyisenge kuikosa Everton FC leo, Raila atua Uingereza

Tuesday November 6 2018

 

By Fadhili Athumani

Nairobi, Kenya. Kambi ya mabingwa wa Ligi Kuu ya Kenya (KPL), Gor Mahia nchini England imepata pigo baada ya kuthibitika kuwa, Straika wake matata, Jacques Tuyisenge, hatokuwepo katika mchezo wa leo kirafiki dhidi ya Everton FC.

Taarifa zilizoifikia Mwanaspoti Digital, zinasema kwamba, Mnyarwanda huyo alipaswa kusafiri siku ya Jumamosi, siku moja baada ya timu kuondoka, amekwama Jijini Nairobi, kutokana na Visa yake kuchelewa. 

Baada ya kushindwa kuondoka nchini siku ya Jumamosi, Tuyisenge alipaswa kuondoka Jumatatu (Novemba 5), lakini kwa bahati mbaya passport yake ambayo ilikuwa imepelekwa Afrika Kusini kwa ajili ya kukamilishwa kwa utaratibu wa kisheria kupita, imebidi aahirishe safari.

Hii inamaanisha kuwa Kogalo itaikosa huduma ya Mshambuliji huyo katika mchezo wa leo usiku, na sasa itabidi Kocha Dylan Kerr, awageukie washambuliaji wake Nicholas Kipkirui, Francis Mustapha, Erissa Sekisambu na Eliud Lokuwam, kuongoza mashambulizi.

Itakumbukwa kwamba, mara ya kwanza zilipokutana (Julai 13, mwaka jana), kwenye Uwanja wa Taifa, Jijini Dar es Salaam, Tanzania, Tuyisenge ndiye aliyefunga bao pekee la kufutia machozi walilolipata Gor Mahia, katika kipigo cha 2-1 walichokipata dhidi ya Everton.

Wakati huo huo, machungu ya kumkosa Tuyisenge katika mchezo huo wa kihistoria, utakaopigwa kuanzia saa 4:00 usiku kwa saa Afrika mashariki, ni kama zitatulizwa na taarifa za uwepo wa Waziri Mkuu wa zamani wa Kenya, Raila Amollo Odinga, uwanjani Goodison Park.

Mbali na Raila aliyetua ambaye ameongozana na binti yake Winnie Odinga, mechi kati ya Kogalo na Toffies, itashuhudia na Mkurugenzi mtendaji wa SportPesa, Captain Ronald Karauri pamoja na maafisa wengine wa kampuni ambao ndio waliodhamini mtanange huo.

Advertisement