Yanga yachomoa, Mayanga wa Ndanda usipime

Muktasari:

Matokeo hayo yanaifanya Yanga kufikisha pointi 26, sawa na Simba inayoshika nafasi ya pili kwa tofauti ya mabao wakati Azam imejikita kileleni ikiwa na pointi 30 baada ya kuichapa Kagera Sugar bao 1-0.

Dar es Salaam. Bao la Rasta Jaffar Mohammed limetosha kuinusuru Yanga na kipigo baada ya kulazimisha sare ya bao 1-1 na Ndanda kwenye kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.

Matokeo hayo yanaifanya Yanga kufikisha pointi 26, sawa na Simba inayoshika nafasi ya pili kwa tofauti ya mabao wakati Azam imejikita kileleni ikiwa na pointi 30 baada ya kuichapa Kagera Sugar bao 1-0.

Ndanda ilikuwa ya kwanza kupata bao dakika 16, lililofungwa na ya mshambuliaji wake Nassor Hashim akimalizia kazi nzuri ya mshambuliaji mwenzake wa Vitalis Mayanga aliyempiga chenga beki wa Yanga, Andrew Vincent ‘Dante’ na kipa Benno Kakolanya kabla ya mfungaji kuuwahi mpira na kumalizia wavuni.

Hata hivyo bao hilo la Ndanda lilidumu kwa dakika 9 tu kabla ya Rasta Jaffar kuisawazishia Yanga akiunganisha kwa kichwa mpira uliopigwa na Ibrahim Ajibu.

Mshambuliaji Ndanda, Mayanga amefunga bao lake la nne msimu huu alikuwa mwiba katika safu ya ulinzi Yanga.

Mayanga alikuwa na kazi kubwa mbele ya Andrew Vicent 'Dante' kwani mara kwa mara walikuwa wakionyeshana ubavu katika uchezaji wao.

Dakika 65 Mayanga alikimbia na mpira na kutaka kuingia ndani ya 18 na kufunga, lakini hata hivyo beki Andrew Vicent aliucheza mpira huo kwa umakini na kipa Kakolanya aliudaka.

Mayanga dakika 85 aliweza kumpita kwa spidi beki Abdallah Shaibu na kufanikiwa kuingia ndani ya 18 lakini hata hivyo Kakolanya alionyesha umahiri wake baada ya kuucheza mpira huo.

Hata hivyo, Yanga nao walionyesha kuhitaji matokeo lakini umakini ulikuwa mdogo baada ya dakika 62 Maka kupiga krosi hata hivyo Makambo alipiga kichwa kilichoenda nje.