#UCHAGUZI SIMBA:Kamati ya Uchaguzi yakabidhiwa kijiti

Muktasari:

Uchaguzi wa Simba unafanyika leo kumaliza miaka minne ya uongozi wa rais Evance Aveva

Dar es Salaam. Kamati Tendaji ya Simba inayomaliza muda wake imekabidhi kijiti kwa kamati ya Uchaguzi tayari kuanza zoezi la kupiga kura.

Kamati ya Uchaguzi ilikabidhiwa kijiti saa 12:40 Mchana huku wanachama wakitakiwa kuchagua viongozi watakaoifanya Simba Sports Club Limited kufika wanakohitaji.

Kaimu rais wa Simba, Salim Abdallah ndiye aliikaribisha kamati ya Uchaguzi iliyoongozwa na Mwenyekiti, Boniface Lyamwike huku akisisitiza wakati huo ndiyo mahala peke iliyokuwa ikisubiliwa na Wanasimba ili kutengeneza mustakabali wa Simba.

Huku akishangilia, Try Again alisema Simba inahitaji kiongozi ambaye ataisaidia klabu siyo yeye asaidiwe na klabu, haitaki kiongozi wa historia kuwa alifanya hiki au kile bali Simba inahitaji kiongozi msafi kiutendaji.

Mwenyekiti wa Try Again aliwambia wanachama wawe makini katika zoezi hilo kwani jukumu ni lao, wasifuate upepo katika kuchagua viongozi.

Baada ya kukabidhiwa kijiti, Lyamwike alianza kutambua uwepo wa viongozi mbalimbali wa klabu hiyo huku akisisitiza zoezi analokwenda kulisimamia litakuwa la kuitoa Simba kutoka ile ya asili hadi ya hisa.

Alisema mwanzoni Simba ilikuwa ni mpira, lakini sasa inakwenda kufanya mpira na biashara hivyo watakaochaguliwa wajue namna ya kutengeneza mipango ya kuiletea Simba faida.