Bao la Kideo la Straika wa Mbao, Ajibu akasome

Muktasari:

Mshambuliaji huyo kati ya mechi 10 walizocheza amefunga mabao manne sawa na nyota wa Simba, Meddie Kagere na kuingia katika orodha ya wafungaji bora hadi sasa akitanguliwa na Eliud Ambokile wa Mbeya City mwenye mabao sita.

Mwanza. Mshambuliaji wa Mbao FC, Said Said amefunga bao la tik-tak lililoipa ushindi timu yake dhidi ya Mtibwa Sugar jambo lililofanya wadau kulilinganisha na lile la Ibrahim Ajibu wa Yanga alilofunga dhidi ya Mbao FC licha ya kwamba hayafanani.

Kocha wa Mbao FC, Amri Said ‘Stam’ akilizungumzia bao la nyota wake Said alisema hadi sasa anaona ndilo bao pekee bora kutokana na mchezaji alivyounganisha mpira huo na kufunga kiufundi.

Alisema mara kadhaa anamuona mshambuliaji huyo kuwa na vitu vya ziada mguuni mwake na hapo baadaye huwenda akawa mchezaji wa kipekee kama ataendelea kutulia na kufuata maelekezo.

“Niwapongeze wachezaji wangu kwa jinsi walivyopambana kupata matokeo mazuri katika mechi ngumu ya leo (jana), lakini niseme bao hili ni bora kati ya mabao yaliyofungwa hadi sasa,”alisema Stam.

Mshambuliaji Said alisema kuwa hakubahatisha kufunga bao hilo, isipokuwa kwa jinsi alivyopokea mpira ilimlazimu kufanya hivyo.

Aliongeza kuwa yeye kama Straika kazi yake ni kufunga bila kujali staili na kwamba malengo yake ni kuisaidia timu kupata matokeo mazuri, lakini kuwania tuzo ya kiatu cha mfungaji bora mwishoni mwa Ligi.

“Naangalia mafanikio ya timu na kujitahidi kuisaidia pamoja na wenzangu, lakini kuhusu bao hili sijabahatisha Straika anafunga kwa staili yoyote na jinsi nilivyoupokea mpira ilinilazimu kufunga hivyo,”alisema nyota huyo.