Mbeya City mzuka umepanda

Muktasari:

Licha ya kuanza vibaya Ligi Kuu, Mbeya City imegeuka kuwa klabu inayoongoza kwa kufunga magoli hivi sasa

Dar es Salaam. Kocha wa Mbeya City, Ramadhan Nswazurwimo amekoshwa na kasi wanayoenda nayo vijana wake baada ya kuanza kwa kusua sua katika Ligi Kuu.

Mbeya City ndio timu pekee inayoongoza kwa kufunga katika Ligi Kuu ikiwa na mabao 12, huku ikitoa mfungaji bora katika Ligi, Eliud Ambokile mwenye goli 6 mpaka hivi sasa.

Nswazurwimo alisema hali hiyo inamfanya aone matunda ya maelekezo yake ambayo alikuwa anatoa wakati walipokuwa wanafanya vibaya mwanzoni.

"Tulianza vibaya Ligi kwahiyo ikawa inanilazimu kuhakikisha kwamba nafanyia marekebisho kikosi changu na tumefanikiwa, nilimwambia Eliud na wenzake walitakiwa kufunga na nashukuru wanafanya hivyo," alisema.

Akizungumzia kuhusu kufanya usajili katika dirisha dogo, alisema kutokana na hali ya uchumi ni ngumu japo kuna sehemu alitamani kufanya marekebisho.

"Timu zote zinalalamika kuhusu ukata wa pesa, kwahiyo sio kama mtu hutaki kufanya usajili hapana ila inabidi ukomae na wachezaji uliopo kwasababu ligi yenyewe ni ngumu haina mdhamini," alisema.