Timu ya Olimpiki yadai baridi iliwakwamisha Argentina

Muktasari:

Imekuwa ni jambo la kawaida kwa wanamichezo wa Tanzania wanapotoka kuwakilisha taifa kwenye mashindano kuja na sababu kadha wa kadha badala ya kuelekeza ukweli kuhusu mbinu za kimchezo zilivyowaangusha.

Dar es Salaam.Wanamichezo walioiwakilisha nchi kwenye Olimpiki ya vijana wamesema kukosa kwao medali kulichangiwa na hali ya hewa nchini Argentina.

Timu hiyo ambayo imewasili leo Jumapili kutoka Argentina imesema hali ya hewa ya baridi ilikuwa kikwazo kwao.

Katika michezo hiyo, Mwanariadha Regina Mpigachai alimaliza wa kwanza katika kundi lake kwenye mbio za mita 800 za raundi ya pili huku raundi ya kwanza akimaliza kwenye nafasi ya saba.

Wakati Francis Damiano alimaliza wa nne kwenye mbio za kilomita 4 alimaliza kwenye  nafasi ya nne na wa 12 kwenye mbio za mita 3,000.

Akizungumza wakati wa kukabidhi bendera kwa Makamu Mwenyekiti wa Kamati ya Olimpiki Tanzania (TOC), Henry Tandau, nahodha wa timu hiyo, Regina Mpigachai alisema kitendo cha kujifua katika mazingira ya joto na kwenda kuchuana kwenye baridi kiliwagharimu.

"Ndiyo sababu mbio za raundi ya kwanza hatukuwa na matokeo mazuri, lakini baada ya kuzoea mazingira tulifanya vizuri," alisema.