Mashabiki Biashara Utd wajipanga kususia mechi

Muktasari:

Mechi ya juzi ya Biashara United dhidi ya KMC ilikuwa ya tano katika Uwanja wa Karume Musoma ambapo Biashara United imepoteza mmoja na kutoa sare nne, matokeo ambayo yamewakatisha tamaa mashabiki.

MUSOMA.  RAHA ya mpira ni ushindi asikwambie mtu,sasa hali imechafuka katika Klabu ya Biashara United baada ya mashabiki kuikatia tamaa timu hiyo na kutishia kutojitokeza uwanjani kuishangilia kutokana na matokeo yasiyoridhisha katika uwanja wa nyumbani.

Timu hiyo ya mkoani Mara ndio msimu wake wa kwanza kushiriki Ligi Kuu lakini imekuwa na mwenendo usioridhisha katika uwanja wake wa Karume mjini Musoma kwa kucheza mechi tano na kuambulia sare nne na kupoteza mmoja.

Kutokana na matokeo hayo mashabiki wameijia juu na kusema kuwa wamekata tamaa kutokana na Chama lao hilo kushindwa kupata ushindi na kuihusisha na kushuka Daraja kama hawatakuwa makini.

Wakizungumza baada ya mchezo wa juzi dhidi ya KMC uliomalizika kwa suluhu ya bila kufungana, baadhi ya mashabiki hao walisema kuwa wamekata tamaa kwa mwenendo wa timu yao.

Hamis Mgendi alisema kuwa mashabiki wamechoka kushuhudia timu yao kuenedelea kupata sare hata kwa timu ndogo na nyingine kupoteza na kwamba inawavunja moyo wanaoacha shughuli zao kuja kuisapoti.

“Sare ya kwanza dhidi ya Azam ilikuwa sahihi,lakini zingine haikuwa sawa kabisa hadi tukafungwa na Mwadui kwa ujumla inatukatisha tamaa sisi mashabiki tunaoacha kazi zetu kuja kuisapoti,” alisema Mgendi.

Naye Manyama Haroun alisema kuwa kutokana na hali hiyo huenda mashabiki wakendelea kupungua uwanjani na kwamba kama juhudi binafsi hazitatumika Biashara United inaweza kushuka Daraja.

“Hata mimi binafsi sitarajii kurudi uwanjani kuishangilia timu hii labda kama itakuwa inacheza na timu kubwa za Simba na Yanga lakini tofauti na hapo siji”alisema Haroun.

Kwa upande wake Kocha wa timu hiyo,Hitimana Thiery alisema kuwa na yeye bado hajajua kwa undani kinachowakosesha ushindi na kudokeza kuwa kiufundi vijana wapo fiti.

“Hata mimi sijui kwa nini tunakosa ushindi,lakini niseme kiufundi wachezaji wapo fiti na mapungufu Bechi langu tunaendelea kuyafanyia kazi,” alisema Kocha huyo raia wa Rwanda.