Kagere, Fei Toto wavunja ukimya

NYOTA wa Yanga, Feisal Salum ‘Fei Toto’ na mshambuliaji wa Simba, Meddie Kagere ni wameamua kuvunja ukimya kwa mara ya kwanza tangu pambano la watani lipigwe wiki tatu zilizopita.

Wachezaji hao ambao waliucheza mchezo huo uliomalizika kwa suluhu ikiwa mara yao ya kwanza, wameuzungumzia uzito wa mchezo huo kwa kulinganisha na walikotokea kabla ya kujiunga na miamba hiyo ya Ligi Kuu Bara.

Kagere, Mnyarwanda mwenye asili ya Uganda anayelichezea taifa la Rwanda alihusika kwenye mchezo mmoja wa dabi akiwa nchini Albania.

Kagere alikuwa akiichezea KF Tirana na Desemba 8, 2014 aliishia benchi kwenye mchezo dhidi ya Partizani Tirana ambao wapo nao kwenye mji mmoja wa Tirana nchini humo.

Akiwa Rwanda, Kagere aliichezea Rayon Sports kwa mwaka mmoja, kuanzia 2013 hadi 2014 na kuhusika kwenye mchezo wa mahasimu kati ya timu yake dhidi ya APR.

Timu nyingine alizozichezea akiwa Rwanda ni ATRACO FC, Kiyovu Sports, Mukura Victory na Police FC. Mshambuliaji huyo, alicheza mashemeji dabi akiwa Kenya ambako aliichezea Gor Mahia kwa miaka mitatu na kukutana na joto wa debi hiyo mbele ya FC Leopard. Baada ya kutua Bongo, alisema mchezo wa watani wa jadi nchini kati ya Simba na Yanga aliuona wa kawaida licha ya kutopachika bao kwenye mchezo huo.

“Nimecheza dabi kubwa sana kwa hiyo ile mechi ya Simba na Yanga haikunisumbua maana kama presha nimekutana nazo kubwa kuliko za hata mchezo huo,” alisema. Kiungo wa Yanga, Feisal Salum ‘Fei Toto’ kwa upande wake licha ya kucheza michezo kadhaa ya mahasimu visiwani Zanzibar, alisema Kariakoo dabi ni kubwa kwenye maisha yake ya soka.