Muindi, Meringor washinda Safaricom Madoka Half Marathon

Muktasari:

Mbio hizo zinazoandaliwa na Mwanasiasa Mkongwe Marsden Madoka, kwa udhamini wa Kampuni ya simu ya Safaricom, yalihusisha mbio za masafa mbalimbali, ambazo ni Kilomita 21 (wanaume na wanawake), Kilomita 10 kwa wakimbiaji chipukizi.

Taita Taveta, Kenya. Daniel Muindi na Delvine Relin Meringor, ndio washindi wa makala ya 13 ya mbio kila mwaka za Safaricom-Madoka Half Marathon, yaliyofanyika jana, Oktoba 20 mjini Ngereny, kaunti ya Taita Taveta.

Muindi alitumia muda wa saa 1:06.04 kuwapiku wapinzani wake, Stephen Mwendwa na George Njoroge, waliomaliza katika nafasi ya pili na tatu, wakitumia muda wa saa 1:06.56 na 1:06:67, kumaliza Kilomita 21.

 “Njia ilikuwa nzuri tu na namshukuru Mungu kwa kuniwezesha kushinda leo. Nilifanya mazoezi ya kutosha na naamini hiyo imenisaidia sana. Kwa sasa najiandaa kwa kushiriki mbio za Bucaramanga, zitakazofanyika nchini Colombia wiki ijayo,” alisema Muindi.

Kwa Upande wake, Meringor ambaye alishiriki mbio hizo kwa mara ya kwanza, alivuka utepe baada ya kukamilisha mzunguko wa Kilomita 21, ndani ya saa 1.16.10, mbele ya Lydia Njeri, aliyemaliza katika nafasi ya pili (1.18.07), akifuatia Esther Chesang (1.19.46).

Katika mbio za Kilomita 10, kwa wanaume, Mshindi alikuwa ni James Mwadime, aliyetumia muda wa dakika 32:38:52. Nafasi ya pili ilienda kwa Gift Bahati, aliyetumia dakika 32:41:26 huku nafasi ya tatu ikienda kwa Mwamburi Jackson, aliyetumia dakika 32:49: 67.

Kwa Upande wa wanawake, Kilomita 10, mshindi alikuwa ni Lucy Mwende, aliyetumia muda wa dakika 50:46:83, sekunde tatu mbele ya Ann Ali (50:49:96) huku Monica Mwende yeye akitumia muda wa dakika 51:20:59, kumaliza katika nafasi ya tatu.