Simba dimbani leo kuvaana na Stand United wakiwa na furaha mfadhili na mdhamini wao, ‘MO’ Dewji kupatikana

Muktasari:

MO Dewji aliyekuwa ametekwa siku tisa zilizopita na watu wasiojulikana, alipatikana usiku wa kuamkia jana baada ya Polisi kueleza kuwa alitelekezwa na watekaji wake katika viwanja vya Gymkhana, Dar es Salaam.

KIKOSI cha Simba, jioni ya leo kinashuka Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam kuvaana na Stand United, huku wakiwa na furaha baada ya mfadhili na mdhamini wao, Mohammed ‘MO’ Dewji kupatikana akiwa hai.

MO Dewji aliyekuwa ametekwa siku tisa zilizopita na watu wasiojulikana, alipatikana usiku wa kuamkia jana baada ya Polisi kueleza kuwa alitelekezwa na watekaji wake katika viwanja vya Gymkhana, Dar es Salaam.

Mfanyabiashara na mwekezaji anayejiandaa kuimiliki klabu ya Simba iliyopo katika mchakato wa kubadilisha mfumo wa wanachama hadi kuwa kampuni ikimilikiwa kwa hisa, alitekwa Alhamisi ya wiki iliyopita akiwa kwenye Hoteli ya Colosseum, Oysterbay anakofanyia mazoezi.

Kutekwa kwa bilionea huyo kuliwafanya Simba kuwa na simanzi na kuendesha dua kila kukicha kumuombea Mo apatikane akiwa salama na dua zao zilijibu baada ya kupatikana kwake jana Jumamosi.

Kupatikana kwa MO kumerejesha shangwe kubwa si kwa familia yake tu, lakini hata kwa viongozi, wachezaji na wadau wengine wa Simba ambao wamekiri hawakuwa na furaha wala amani tangu tukio hilo lilipotokea.

BABA MTU AFICHUA

Baba wa bilionea huyo, Gullam Dewji, alifichua jinsi alivyompata mwanaye kwa kueleza kuwa, alipigiwa simu kuwa, MO ameonekana Gymkhana jijini Dar es Salaam ndani ya gari.

Gullam alisimulia, lakini MO mwenyewe aliposhushwa katika gari la wanaodaiwa watekaji wake, alitembea kutafuta msaada wa mawasiliano ili azungumze na familia yake kuwajulisha mahali alipo.

Alisema baada ya kupokea simu hiyo alifika haraka eneo la tukio na kumpata MO na alimshukuru Mungu kwa kumrejesha akiwa salama na haraka alimfikisha nyumbani akiwa na majeraha kidogo, ila muhimu kwake MO kuwa yu hai.

“Niliwajulisha Polisi juu ya kupatikana kwa mwanae nao walifika nyumbani Oysterybay. Kwa kweli tunamshukuru Rais John Magufuli kwa kufanikisha kupatikana kwa kijana wangu, pia nawapongeza Polisi kwa kazi kubwa waliyoifanya.”

MO HUYU HAPA

Bilionea huyo hakupenda kuzungumza sana badala yake alimshukuru Mungu kwa kumrejesha salama, huku akionekana kudhoofu na ndevu zikiwa zimemuota kwa fujo usoni mwake, akiwa kavaa tisheti fulani ya kichovu hivi.

Pia, kupitia akaunti ya Twitter ya Kampuni ya Mohamed Enterprise Limited (Metl Group) aliandika; “Namshukuru mwenyezi Mungu nimerudi salama nyumbani. Nawashukuru Watanzania wenzangu na watu wote kote duniani kwa dua na sala zao. Nashukuru mamlaka zote, ikiwemo Jeshi la Polisi, zilizofanya kazi ya kuhakikisha narudi salama.”

Naye msemaji wa familia Azim Dewji alisema MO amepatikana akiwa na afya njema kwa asilimia 100, labda tu suala la kuvurugwa kisaikolojia kwa tukio lililompata na ndio maana wametaka apumzike kwanza.

“Amepatikana muda wa saa 8.30 usiku, walimuacha halafu yeye (MO) akapiga simu kwa baba yake. Tunamshukuru sana Rais Magufuli) kwa kuagiza vyombo vyake vya usalama, tumempata,” alisema Azim.

Mapema jana asubuhi ilielezwa kuwa familia hiyo ingezungumza na wanahabari, lakini baadaye waliahirisha baada ya Ghullam kueleza kuwa, wanahitaji kupumzika kwani siku tisa za kutowekwa kwa MO hazikuwa na amani hivyo, anahitaji kupumzika ili kujiweka fiti kabla ya kueleza kilichomkuta.

POLISI HAWA HAPA

Kamanda wa Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam, Lazaro Mambosasa na Mkuu wa Jeshi la Polisi (IGP) Simon Sirro walithibitisha kwa nyakati tofauti juu ya kupatikana kwa MO na kwamba, wanaendelea kuwasaka wahusika.

“Tulipata taarifa amepatikana, watekaji walimchukua katika gari ile ile lililotumika kumteka na kwenda kumtupa Gymkhana,” alisema Mambosasa.

“Tangu alivyotekwa pale Colosseum gari ya watekaji iliondoka kasi na baada ya dakika 15 Dewji alijikuta amewekwa kwenye chumba akiwa amefunikwa ili asiwatambue watekaji,” alisisitiza Kamanda Mambosasa.

“Baada ya kumhoji ameeleza kuwa alitambua lugha walizokuwa wakizungumza kwamba ni kama za Afrika Kusini. Shaka yetu kuwa waliofanya tukio hili sio Watanzania yamethibitishwa na MO mwenyewe.”

SIMBA MZUKA

Nyota wa Simba pamoja na benchi la ufundi na wadau wengine wa klabu hiyo wameonyesha furaha yao kwa MO kupatikana na kuahidi kufanya kweli kwenye mchezo wao leo dhidi ya Stand United.

Nahodha Msaidizi Mohammed Hussein ‘Tshabalala’ alisema morali ya jeshi lake imeongezeka na wamejipanga kushinda leo ili kupata pointi tatu.

“Kwangu naomba nizungumzie zaidi mechi na Stand wachezaji wote tuna morali ya hali ya juu kuhakikisha tunashinda mechi hii ili kuwa katika mazingira mazuri kwenye msimamo wa ligi,” alisema Tshabalala.

Beki Paul Bukaba alisema morali ni kubwa kambini tangu zifike taarifa za kupatikana kwa MO, huku kipa Deo Munishi ‘Dida’ akisema wanataka kuutumia mchezo wa leo kama kutoa pole kwa bilionea wao huyo.

“Ni furaha kubwa kwa sababu ni mtu, ambaye tunamtegemea kama unavyojua, sasa akili imetulia kwa sababu awali mambo yalikuwa magumu mazoezi tulikuwa tunafanya hivyo tu,” alisema Dida, ambaye pia aliwahi kuzichezea Yanga, Mtibwa Sugar na Azam FC.

Kwa upande wao, Yusuf Mlipili, James Kotei na Kocha wa Viungo, Adel Zrane walisema wamefarijika sana kurejea kwa Mo, huku kina Hassan Dalali na viongozi wa klabu nyingine wakishukuru Mungu kwa kupatikana kwa bilionea huyo. Simba inashuka uwanjani saa 10 jioni kuvaana na Stand katika mchezo wa nane kwao msimu huu, huku wakiwa na kumbukumbu ya ushindi wa mabaio 2-1 iliyopata mbele ya Africans Lyon. Wekundu wanahitaji ushindi ili kuwasogelea watani zao ambao jana wamechomoza na ushindi wa mabao 3-0 dhidi ya Alliance, pia kupunguza pengo la pointi dhidi ya vinara Azam wanaoongoza msimamo.

IMEANDIKWA NA KHATIMU

NAHEKA, IBRAHIM YAMOLA, DORIS MALIYAGA,CHARITY JAMES, OLIPA ASSA NA THOBIAS

SEBASTIAN