AJIRA: Hawa wote wanatosha kumbadili Mourinho

MANCHESTER, ENGLAND. JOSE Mourinho ndio kama ulivyosikia. Mambo yake huko Manchester United kila kukicha ni presha tu. Mechi ile ya Newcastle United ilishusha presha kidogo, lakini hapo jana Jumamosi alikuwa na shughuli pevu nyingine huko Stamford Bridge wakati kikosi chake kilipokwenda kuikabili Chelsea ya Eden Hazard kwenye Ligi Kuu England.

Si jambo la kificho kwamba Man United kwa sasa hakuna matokeo mengine yanayokubalika zaidi ya ushindi tu, kinyume cha hapo basi ni presha isiyokwisha kwa Mourinho na kibarua chake kuwekwa rehani. Kuna makocha hao wanatajwa kwamba kama Mourinho kazi itamshinda, basi hawa wananweza kuwa msaada kutokana na ubora wao na namna watakavyowatumia mastaa wa timu hiyo kubadili hali ya mambo.

PAULO FONSECA

Fonseca amekuwa kocha wa Shakhtar Donetsk mwaka 2016. Katika msimu wake wa kwanza tu kwenye timu hiyo alibeba mataji muhimu huko Ukraine. Katika msimu wake wa pili aliongoza timu hiyo kwenye Ligi ya Mabingwa Ulaya na kuwachapa Manchester City na Napoli kwenye msimu huo. Mfumo wake anaopendelea ni 4-2-3-1, huku mabeki wa kati akiwapanga pembeni, huku kiungo wa kati akirudi nyuma zaidi na mabeki wa pembeni wanatumika kama mawinga, ambao wakati mwingine wanaingia katikati ya uwanja kwenda kucheza kama viungo. Kwa kutumia mfumo huo, Shakhtar imekuwa timu tishio na kuwa na umri mkubwa wa mpira ndani ya uwanja, ambapo kwa msimu wote uliopita walikuwa na asilimia 62.3 ya umiliki wa mpira kwa mujibu wa data za Wyscout. Mfumo huo wa Fonseca utamfanya Fred atambe kwenye kikosi cha Man United kama kocha huyo atatua Old Trafford kuchukua mikoba ya Mourinho.

RALPH HASENHUTTL

RB Leipzig waliikamatia Bundesliga kwenye msimu wa 2016/17. Wamekuwa na ubora mkubwa sana tangu walipopanda kwenye ligi hiyo na kuhamia makali yao hadi kwenye michuano ya Ulaya. Hasenhuttl, aliwahi kuinoa pia Ingolstadt na mambo yao yalikuwa moto kwelikweli. Fomesheni inayopendelewa na kocha huyo wa Austria ni 4-2-2-2, ikiwa na lengo la kumdhibiti mpinzani akiwa kwenye eneo lake la nyuma kabisa. Aliwafanya wachezaji kama Naby Keita, Timo Werner na Emil Forsberg kuwa mahiri zaidi, hivyo akija kwenye kikosi cha Man United atakwenda kuwabadili mastaa wa timu hiyo na kufanya vyema zaidi uwanjani. Timu ya Hasenhuttl huwa haifungwi hovyo hovyo kutokana na uhodari wake wa kutengeneza beki ya kibabe.

MAURICIO POCHETTINO

Ndani ya miaka minne, Pochettino ameibadili sana Tottenham Hotspur kutoka kuwa timu ya kawaida na kuwa timu inayoshindania ubingwa. Katika kipindi chake alichokuwa kwenye kikosi hicho, Spurs imekuwa timu tofauti na hata kuwapiku mahasimu wao Arsenal kwenye msimamo wa ligi kwa misimu miwili mfululizo na kutamba huko kwenye Ligi ya Mabingwa Ulaya. Kocha huyo ni hodari na ni mtu sahihi kama atakwenda kupewa mikoba ya kuinoa Man United iliyopo chini ya Mourinho kwa sasa. Muargentina huyo ni mpenzi wa wachezaji vijana, hivyo kama atatua Old Trafford basi utakuwa wakati mwafaka wa wachezaji kama Marcos Rashford na Anthony Martial kupewa nafasi ya kutamba kwenye kikosi hicho.

BRENDAN RODGERS

Inachangaza kwaninni Rodgers hapewi thamani yake inayostahili kama mmoja wa makocha mahiri. Kocha huyo amefanya makubwa Watford, Swansea City na hata Liverpool alikokaribia kabisa kubeba ubingwa wa Ligi Kuu England. Na sasa kwa misimu miwili yupo Celtic na wapo vizuri kweli kweli. Soka la Rodgers ni kushambulia na lenye mvuto kitu ambacho ndicho wanachokikosa Man United kwa sasa kutokana na kocha wao Mourinho kufikiria zaidi kwenye kukaba. Man United imekuwa timu ya kukaba tu na si kucheza soka la kushambulia na jambo hilo linawavuruga sana mashabiki wa wababe hao wa Old Trafford. Rodgers ana uwezo mkubwa sana wa kuongezea wachezaji viwango na akitua Old Trafford watu kama Alexis Sanchez wataanza kuonyesha makali yao ndani ya uwanja.

MARCO ROSE

Katika msimu wake wa kwanza kwenye ukocha wa hadhi ya juu, Rose aliifikisha Red Bull Salzburg nusu fainali ya Europa League. Wakati anafika hatua hiyo, timu kama Marseille, Lazio, Dortmund na Real Sociedad zote alizichapa. Fomesheni yake anayopenda kutumia Rose ni 4-3-1-2, huku akiwa na kawaida ya kutengeneza miundo ya kombinesheni tofauti kwenye sehemu ya kiungo. Rose anafundisha soka kama laa Jurgen Klopp kukabia huko huko juu kwa wapinzani huku akihakikisha kwamba wachezaji wake wajaribu kurudisha mpira kwenye himaya yao haraka sana pindi wanapoupoteza. Akitua Old Trafford atakwenda kuwatumia ipasavyo mastaa kama Romelu Lukaku, Jesse Lingard na Paul Pogba kwa sababu ndio wachezaji wake anaowahitaji.

ZINEDINE ZIDANE

Zidane kwa sasa ndiye kocha mwenye jina kubwa ambaye hana kazi sambamba na Arsene Wenger. Jambo hilo ndio maana majina yao yamekuwa hayakauki kwenye kuhusishwa na timu nyingi hasa huko Man United kwenye kiti cha Mourinho. Kuhusu Zidane, kile alichokifanya Real Madrid kinajieleza bayana akiweka rekodi ya kubeba ubingwa wa Ligi ya Mabingwa Ulaya kwa misimu mitatu mfululizo. Amebeba mataji ya kutosha tu, hivyo ni mtu asiyekuwa na mashaka kama mabosi wa Man United wataamua kumpa kazi anayofanya Mourinho huko Old Trafford.