WAKALI: Wanaofunika kwa mishahara ya timu zote England

LONDON, ENGLAND. SI jambo la siri kwamba wanasoka wanavuna pesa nyingi sana. Baadhi wanalipwa inavyostahili, lakini wengine wanalipwa pesa nyingi zaidi.

Jambo hilo linafanya kila kijana kukua na ndoto za kuwa mwanasoka wa kulipwa kwa sababu ni kazi itakayompatia pesa nyingi huku akifanya mchezo anaoupenda.

Kwa inavyoendelea kwa sasa kwenye soko la mchezo huo unaweza kuona bayana. Beki wa kushoto wa Manchester United, Luke Shaw hivi karibuni amesaini mkataba mpya wa miaka mitano wa kuitumikia timu hiyo ya Old Trafford. Mkataba huo mpya unamshuhudia Shaw akilipwa Pauni 195,000 kwa wiki. Kwa mshahara huo, Shaw sasa anakuwa mchezaji wa tano anayelipwa pesa ndefu huko Man United na wachezaji wanaomzidi ni David De Gea, Paul Pogba, Alexis Sanchez na Romelu Lukaku.

Lakini, unataka kufahamu ni mchezaji gani anayelipwa mshahara mkubwa katika kila klabu ya Ligi Kuu England? Hawa ndio wanaoongoza kwa kulipwa mishahara mikubwa kwa wiki katika kila klabu ya Ligi Kuu England.

Arsenal- Mesut Ozil, Pauni 350,000 kwa wiki

Kiungo wa Kijerumani, Mesut Ozil ndiye mchezaji anayelipwa mshahara mkubwa zaidi kwenye kikosi cha Arsenal baada ya kuripotiwa kwamba anapokea Pauni 350,000 kwa wiki. Ozil alisaini mkataba mpya Februari mwaka huu na atakuwa na Arsenal tangu Juni 2021 na kwamba ndiye mchezaji anayelipwa mshahara mkubwa zaidi katika historia ya timu hiyo.

Bournemouth- Jermain Defoe, Pauni 100,000 kwa wiki

Straika, Jermain Defoe ndiye mchezaji anayelipwa mshahara mkubwa kwenye kikosi cha Bournemouth baada ya kuripotiwa kwamba anapokea zaidi ya Pauni 100,000 kwa wiki kwenye kikosi hicho cha kocha Eddie Howe. Hata hivyo, straika huyo hakuwa ameanza kwenye mechi yoyote ya Ligi Kuu England msimu huu hadi kufikia jana Jumamosi na ametumika mara mbili tu akitokea benchi.

Brighton- Jose Izquierdo, Pauni 45,000 kwa wiki

Kwenye kikosi cha Brighton kuna wachezaji wawili wanaolingana kwa mishahara Jose Izquierdo na Jurgen Locadia na hao ndio wanaolipwa pesa ndefu zaidi. Ripoti zinadai kwamba wachezaji hao kila mmoja kwa wiki analipwa Pauni 45,000 kutokana na huduma zao wanazotoa kikosini. Izquierdo alijiunga na timu hiyo mara tu baada ya kupanda daraja, wakati Locadia alitua hapo kwenye dirisha la Januari mwaka huu.

Burnley- Chris Wood, Pauni 35,000 kwa wiki

Burnley inanolewa na kocha Sean Dyche. Kikosi hicho kina wachezaji sita wanaolipwa mshahara unaolingana, ambao ndio hasa mkubwa kwenye klabu hiyo. Wachezaji hao sita wakiongozwa na Chris Wood ni Robbie Brady, Jack Cork, Steven Defour, Tom Heaton na Jeff Hendrick. Burnley inawalipa mastaa wake hao Pauni 35,000 kwa wiki kwa kila mchezaji na ndio wachezaji wao wanaopokea mkwanja mrefu.

Cardiff- Harry Arter, Pauni 40,000 kwa wiki

Kwenye kikosi cha Cardiff City mchezaji anayelipwa mshahara mkubwa ni Harry Arter, ambaye yupo kwenye kikosi hicho kwa mkopo. Cardiff imerejea kwenye Ligi Kuu England msimu huu na kikosi hicho cha kocha Neil Warnock kinaelezwa kwamba ni timu yenye bili ndogo zaidi ya mishahara kuliko zote kwenye Ligi Kuu England. Mchezaji wao anayelipwa mshahara mkubwa wanamlipa Pauni 40,000 kwa wiki.

Chelsea- Eden Hazard, Pauni 200,000 kwa siki

Si jambo la kushangaza kusikia kwamba Eden Hazard ndiye mchezaji anayelipwa mshahara mkubwa zaidi huko Stamford Bridge. Imeripotiwa kwamba Hazard anataka kusaini mkataba mpya ambao utamfanya awe anavuta pesa ndefu zaidi kwa wiki, lakini kwa mkataba huu wa sasa staa huyo wa Kibelgiji analipwa Pauni 200,000 kwa wiki. Anastahili mshahara huo kutokana na huduma yake matata.

Crystal Palace- Wilfried Zaha, Pauni 130,000 kwa wiki

Kama ilivyo tu huko Chelsea, si kitu kinashangaza kwa staa Wilfred Zaha kuongoza kwa kulipwa mshahara mkubwa kwenye kikosi cha Crystal Palace. Winga huyo wa kimataifa wa Ivory Coast alisaini mkataba mpya kwenye majira ya kiangazi mwaka huu ambapo atakuwa kwenye timu hiyo hadi 2023. Mshahara wake anaotajwa kuwa mkubwa, Zaha analipwa Pauni 130,000 kwa wiki.

Everton- Gylfi Sigurdsson, Paunni 150,000 kwa wiki

Kiungo mchezeshaji Gylfi Sigurdsson ndiye anayeongoza kwa kulipwa mshahara mkubwa huko kwenye kikosi cha Everton kutokana na kupokea Pauni 150,000 kwa wiki. Mchezaji mwingine kwenye kikosi hicho anayepokea mshahara kama huo ni staa mpya Bernard. Kumekuwa na ripoti kwamba huenda mchezaji Richarlison naye akapokea kiwango kama hicho cha mshahara tangu aliponaswa kwa Pauni 50 milioni akitokea Watford.

Fulham- Aleksandar Mitrovic, Pauni 50,000 kwa wiki

Fulham wameamua kuweka viwango vyao vya mishahara chini, lakini straika wao wa Kiserbia Aleksandar Mitrovic anakula pesa ndefu kwa wiki. Staa huyo ameripotiwa kwamba analipwa Pauni 50,000 kwa wiki. Kiwango hicho cha pesa kinaendana na huduma ya mchezaji huyo kwenye kikosi hicho ambapo kabla ya mechi za jana alikuwa ametupia wavuni mara tano kwenye Ligi Kuu England.

Huddersfield- Alex Pritchard, Pauni 110,000 kwa wiki

Huddersfield mambo yao si mazuri kwenye Ligi Kuu Enngland msimu huu. Lakini, hilo halina maana kwamba waache kutoa mishahara mikubwa na ripoti zinafichua kwamba Alex Pritchard ndiye anayelipwa mshahara mkubwa zaidi, Pauni 110,000 kwa wiki. Mchezaji huyo alitua hapo akitokea Norwich City kwenye dirisha la Jannuari, licha ya kwamba huduma yake haivutii sana.

Leicester City- Jamie Vardy, Pauni 100,000 kwa wiki

Kwenye kilele cha mishahara ya Leicester City, straika Jamie Vardy ndiye anayeoongoza kwa kulipwa pesa ndefu. Staa huyo wa kimataifa wa England analipwa Pauni 100,000 kwa wiki. Vardy ni mmoja wa wachezaji muhimu sana kwenye kikosi hicho kilichobeba ubingwa wa Ligi Kuu England katika msimu wa 2015-16 na ndio maana hata mshahara wake umekuwa mkubwa kuliko wengine.

Liverpool- Mo Salah, Pauni 200,000 kwa wiki

Mohamed Salah alisaini mkataba mpya kwenye kikosi cha Liverpool mwishoni mwa msimu uliopita baada ya kufunga mabao 32 kwenye ligi msimu uliomalizika na kubeba Kiatu cha Dhahabu. Mkataba huo mpya unamfanya Mo Salah kulipwa Pauni 200,000 kwa wiki na hivyo kuwa mchezaji anayepokea pesa ndefu zaidi katika kikosi hicho kinachonolewa na Jurgen Klopp huko Anfield.

Man City- Kevin de Bruyne, Pauni 350,000 kwa wiki

Kevin De Bruyne anaongoza kwenye orodha ya mishahara huko kwennye kikosi cha Manchester City. Staa huyo wa Kibelgiji analipwa Pauni 350,000 kwa wiki na kuwa mchezaji anayelipwa zaidi katika kikosi hicho cha Etihad. Kocha, Pep Guardiola hana mashata kumpa mshahara huo mchezaji huyo kutokana na huduma yake bora anayotoa uwanjani ambao msimu uliopita tu aliipa timu hiyo ubingwa wa Ligi Kuu Englannd.

Man United- Alexis Sanchez, Pauni 500,000 kwa wiki

Staa wa zamani wa Arsenal, Alexis Sanchez ndiye mchezaji ananyelipwa mshahara mkubwa huko Manchester United licha ya kucheza kwa kiwango cha chini. Mshambuliaji huyo wa kimataifa wa Chile analipwa Pauni 500,000 kwa wiki na hakika huduma yake bado haijaleta mafanikio makubwa huko Old Trafford na kumfanya kocha aliyemsajili, Jose Mourinho kuwa kwenye presha kubwa ya kupoteza ajira yake.

Newcastle United- Jonjo Shelvey, Pauni 70,000 kwa wiki

Huko kwenye kikosi cha Newcastle United mambo yamekuwa ya hovyo kweli kweli hasa kutokana na mambo ya mmiliki wa timu hiyo kushindwa kufanya usajili wa mchezaji wa maana kwenye timu. Kwa nyota waliopo kwenye timu hiyo, kiungo Jonjo Shelvey, ndiye anayelipwa mshahara mkubwa kutokana na kupokea Pauni 70,000 kwa wiki kwa huduma yake anayotoa St James’ Park.

Southampton- Manolo Gabbiadini, Pauni 80,000 kwa wiki

Licha ya mshambuliaji Danny Ings kutua kwennye timu hiyo kwa mkopo akitokea Liverpool, Manolo Gabbiadini bado anaongoza kwa kulipwa mshahara mkubwa huko St Mary’s kutokanana kupokea Pauni 80,000 kwa wiki. Straika huyo wa Kitaliano amekuwa na mchango mzuri kwenye kikosi hicho, lakini mambo yake kwa siku za karibuni yamekuwa hayatishi sana kutokana na kuwa kwenye kiwango cha chini sana cha fomu yake ya uwanjani.

Tottenham- Harry Kane, Pauni 200,000 kwa wiki

Si kitu kinachoshangaza kumwona straika Harry Kane akiwa kinara wa mshahara huko kwenye kikosi cha Tottenham Hotspur. Mwingereza huyo analipwa mshahara wa Pauni 200,000 kwa wiki. Kane ni mshambuliaji mwenye uhakika wa kupiga mabao licha ya kwamba kwa msimu huu mambo yake yamekuwa magumu kwenye Ligi Kuu England na michuano minginne kutokana na kupungua kasi yake ya kufunga mabao.

Watford- Andre Gray, Pauni 70,000 kwa wiki

Andre Gray analipwa mshahara wa Pauni 70,000 kwa wiki huko Vicarage Road na kumfanya kuwa na mshahara mkubwa kuliko wote katika kikosi cha Watford. Fowadi huyo ameunga kombinesheni bomba sambamba na Troy Deeney na kuwa tishio sana mwanzoni mwa msimu huu. Lakini, huduma ya Gray ndiyo inayomfanya alipwe mshahara mkubwa kwenye kikosi hicho cha Watford.

West Ham- Chicharito, Pauni 140,000 kwa wiki

Straika, Javier Hernandez maarufu kwa jina la Chicharito ndiye mchezaji anayelipwa mshahara mkubwa kwenye kikosi cha West Ham United. Hata hivyo, Chicharito ameshindwa kuonyesha yale makali yake ya kufunga mabao tangu alipojiunga na timu hiyo licha ya kulipwa mshahara mkubwa kuliko wengine kutokana na kupokea Pauni 140,000 kila wiki.

Wolves- Ruben Neves, Pauni 50,000 kwa wiki

Jina jingine lisiloshangaza kuona linalipwa mshahara mkubwa kwenye timu yake baada ya Ruben Neves kulipwa Pauni 50,000 kwa wiki huko Molineux. Kiungo huyo wa Kireno huduma yake anayotoa katika kikosi cha Wolves ni kubwa na ndio maana haishangazi kuona analipwa mshahara huo mkubwa kuliko wachezaji wengine kwenye timu hiyo. Neves amekuwa shida na Wolves wanakabiliwa na vita kali ya kumzuia asinaswe na vigogo.