Fred The Red na vikalagosi wengine maarufu kwenye Ligi Kuu England

LONDON, ENGLAND. KAWAIDA kwenye mchezo wa soka kwa timu au michuano fulani kuwa na vikalagosi vya kupambana timu hizo au michuano hiyo kwa kuburudisha mashabiki wake uwanjani.

Kwenye Ligi Kuu England kuna timu nyingi sana zimekuwa na vikalagosi ambao, wamekuwa wakiwatumia kwenye mechi zao za nyumbani ili kutoa burudani kwa mashabiki wao kabla ya mechi zao za nyumbani kuanza.

Hata hivyo, kuna vikalagosi wa timu tano tu ndio waliokuwa maarufu zaidi kwenye Ligi Kuu England kutokana na kupendwa na mashabiki wa timu mbalimbali. Hawa hapa ndio vikalagosi maarufu kwenye Ligi Kuu England kwa sasa.

5.Tottenham- Chirpy na Lily

Kama Chelsea tu, Tottenham Hotspur nao ina vikalagosi wawili. Wababe hao wa London wameamua kuwaita vikalagosi wao hao majina ya Chirpy na Lily. Wamekuwa wakionekana pamoja katika kila mechi za nyumbani za Spurs na hakika jambo hilo limekuwa likiwapa burudani kubwa mashabiki wa timu hiyo. Vikalagosi hao wa Spurs ni moja kati ya walio maarufu zaidi kwenye Ligi Kuu England na mashabiki wamependa kukutana nao na kupiga nao picha.

4.Chelsea-

Stamford na Bridget

Stamford ni simba dume na Bridget ni simba jike. Hao ni vikalagosi wa Chelsea huko Stamford Bridge. Mashabiki wa Chelsea wanawafahamu vikalagosi wao na kwamba, wamekuwa na staili tofauti kwa sababu klabu nyingine zinatumia kikalagosi mmoja, zenyewe inao wawili. Vikalagosi hao wanaitwa Stamford, ambaye ni simba dume na Bridget ambaye ni simba jike. Simba dume alikuwa mwenyewe tu klabuni hapo Stamford Bridge hadi 2013 hadi hapo Chelsea walipomtambulisha kikalagosi wa kike kupeana sapoti. Jambo hilo limeonekana kubamba vyema na mashabiki wa timu hiyo wamelipenda wazo hilo.

3.Liverpool-

Mighty Red

Mashabiki wa Liverpool duniani kote wanamfahamu vyema kikalagosi wao, Mighty Red. Kikalagosi huyo ana mwonekano kama wa ndege, lakini sasa yeye ana meno jambo linalomfanya kuwa maarufu kwamba ndege mwenye meno. Mighty Red amekuwa maarufu sana huko Anfield na mashabiki wanaokuwa kwenye majukwaa ya timu hiyo wamekuwa wakipenda kujichanganya na kituko wao huyo anayewafurahisha uwanjani ukiweka kando yale mabao ya akina Mohamed Salah na mwenzake Sadio Manne.

2.Arsenal-

Gunnersaurus

Tangu mwaka 1994, kikalagosi wa Arsenal, Gunnersaurus Rex amefanya kazi kubwa sana ya kuburudisha mashabiki wanaokuja uwanjani kuitazama timu hiyo ikicheza inapokuwa kwenye mechi zake za nyumbani. Mashabiki wa Arsenal wanapenda sana kupiga picha na kuzungumza na kikalagosi hiyo katika kila mechi wanazokuwa nyumbani. Kutokana na urafiki nna umaarufu wake kwa mashabiki hao, Arsenal wameamua kufungua kurasa za mitandao ya kijamii inayomhusu kikalagosi huyo tu.

1.Man United-

Fred The Red

Kikalagosi wa Manchester United, Fred the Red, kwa miaka kadhaa amekuwa akipigiwa kura kuwa ndiye maarufu zaidi kwa vikalagosi wa Ligi Kuu England. Mashabiki wa wababe hao wa Old Trafford wamekuwa wakimpenda sana kikalagosi wao na kupiga naye picha kila wakati wa mechi za timu hiyo. Wakati Jose Mourinho anatua kwenye kikosi hicho kulikuwa na maelezo kwamba huenda akambadilisha kikalagosi huyo, lakini wawili hao wamekuwa marafiki kwa sasa.