Maisha ya mastaa Simba ndani ya Mtibwa Sugar

Muktasari:

  • Wachezaji hao waliachwa na Simba msimu wa 2018/19, wameamua kukubaliana na hali halisi na kuona ndoto zao zitafanikiwa kwenye klabu zao mpya.

Dar es Salaam. Maisha ya wachezaji walioachwa na Simba, Ally Shomari na Juma Luizio yameanza kuonyesha nuru ya kurudisha ndoto zao ndani ya kikosi cha Mtibwa Sugar.
Akizungumzia maisha yake mapya ndani ya Mtibwa Sugar, Shomari alisema ameanza kuona mwanga wa ndoto yake ya kulinda kiwango chake.
Simba ilimsajili Shomari msimu uliopita na walichana naye mwaka huu ambapo akaamua kurejea Morogoro kwenye klabu yake ya zamani Mtibwa Sugar ambako kocha Zuber Katwila anampa nafasi ya kucheza, inayomfanya ajiamini na kuona ndoto zake zinarejea.
Shomari alisema alipokuwa Simba alipata changamoto ya kukosa namba ndani ya kikosi cha kwanza na kufanya ashindwe kuelewa kama kiwango chake kinapanda.
"Kiwango cha mchezaji kinatokana na kucheza mechi nyingi kama ninayopata Mtibwa Sugar kwa sasa, lakini kukaa benchi inafifisha ari ya kujiamini, kuthubutu na kujituma kwa bidii.
"Bahati nzuri Mtibwa Sugar mwaka huu inashiriki michuano ya Kombe la Shirikisho Afrika itakayotupa nafasi wachezaji kuonyesha uwezo wetu kwenye timu za nje," alisema Shomari.
Naye Luizio aliyerejea Mtibwa Sugar kwa mara nyingi amesema kwake popote ni kambi kinachotakiwa ni kujituma kwa bidii.
"Mchezaji hawezi kuchagua timu kinachotakiwa ni huduma yake kuwa msaada ndani ya timu husika iliyomsajili," alisema mshambuliaji huyo.