Familia: Ukifichua MO alipo unavuta bilioni 1

Muktasari:

MO Dewji, aliyepitishwa kwa kauli moja na wanachama wa Simba kuwa mwekezaji wa klabu hiyo iliyopo kwenye mchakato wa kuendeshwa kisasa kwa mfumo wa hisa, alitekwa alfajiri ya Alhamisi iliyopita katika hoteli ya Colosseum alipokuwa amekwenda kwa ajili ya mazoezi ya viungo na hadi sasa hajajulikana mahali alipo.

WAKATI mabosi, wanachama na mashabiki wa Simba wakiendelea kumlilia Mungu na kuangusha dua, ili mfadhili na mdhamini wao, Mohammed ‘MO’ Dewji  apatikane akiwa salama, familia ya bilionea huyo imetangaza bingo ya maana.

Hata hivyo, jana familia ya MO Dewji, ilitangaza dau nono la Shilingi 1 bilioni kwa yeyote atakayefanikisha kutoa taarifa za kupatikana kwa mpendwa wao.

Tamko hilo la kwanza kwa familia tangu kutekwa kwa MO lilitolewa na Msemaji wa Familia, Azim Dewji aliyekuwa ameambatana na baba wa bilionea huyo, Ghulam Dewji sambamba na Meneja Miradi ya Kampuni za METL, Sudi Mwanasala.

“Familia inaahidi kwamba mtoa taarifa pamoja na taarifa zake zitabaki kuwa za siri kubwa baina yake na familia,” alisema Azim mfadhili wa zamani wa klabu hiyo aliyeisaidia kuifikisha Simba Fainali za Kombe la CAF-1993 na kulikosa taji kiduchu baada ya kufungwa mabao 2-0 na Stella Abidjan ya Ivory Coast katika mchezo wa marudiano wa fainali hiyo kufuatia suluhu ya ugenini kwenye mchezo wa kwanza.

Azim alianika namba ambazo zitatumika kupitisha taarifa kuwa ni 0755-030014, 0717-208478, 0784-783228 au barua pepe [email protected].

Aidha familia hiyo iliishukuru Serikali pamoja na vyombo vya dola kwa kulipa uzito tatizo hilo.

BABA MTU HUZUNI TUPU

Katika mkutano huo usingependa kumwangalia mara mbili baba yake mzazi wa MO Dewji, Ghulam Dewji kutokana na kuwa na uso wa huzuni wakati wote.

Ghulam alianza kuonekana mapema katika varanda za jengo hilo la ofisi zake akiwa na pilikapilika za huku na kule.

Baada ya muda Ghulam alionekana akizungumza na Azim kisha kuingia naye katika moja ya ofisi zake.

Wakati wote uso wake ulikuwa wa majonzi makubwa kutokana tukio la kutekwa kwa mwanaye huyo.
Aidha mfanyabiashara huyo mkubwa licha ya wasaidizi wake kusema asingeweza kufika mkutano huo kutokana na kutokuwa na hali nzuri lakini alifika aliongozana na Azim na Meneja Miradi ya Kampuni za METL, Sudi Mwanasala katika mkutano huo. Wakati wote wa mkutano huo, Mzee Ghulam alionekana katika uso wa majonzi makubwa huku akijaribu kufuatilia kile kilichokuwa kikisomwa na Azim.

Mara baada ya mkutano huo Ghulam alionekana kutikisa kichwa mara mbili huku akifarijiwa na Azim.
Mbali na Ghulam hali ya majonzi ilikuwa pia kwa wafanyakazi wa kampuni hiyo ambao kila mmoja hakuwa katika uchangamfu kama ilivyozoeleka katika mikutano ya MO iliyopita.