Joshua asherehekea kuzaliwa kwake kimtindo

Muktasari:

Joshua ameshinda mapambano yake yote 22 ya ngumi za kulipwa aliyocheza huku akishinda 21 kwa KO na moja pekee ndilo ameshinda kwa pointi.

London, England. Bondia bingwa wa Dunia uzani wa juu, Anthony Joshua, jana aliungana na marafiki na jamaa zake wa karibu kwa kuwasha mshumaa aliouita wa matumaini katika sherehe ya kuzaliwa kwake.

Bondia huyo alisherehekea kutimiza miaka 29, tangu kuzaliwa kwake kwa kuwasha mshumaa huo wa matumaini kabla na kutamba kuwa ni dalili njema kwake kwamba ataendelea kumeremeta kwa kipindi kirefu kijacho.

Joshua alitwaa ubingwa huo wa Dunia baada ya kumchapa Alexander Povetkin wa Russia kwa KO na kutwaa mataji ya WBO, WBA na IBF sasa anasubiri kucheza pambano la kuunganisha mikanda atakapocheza na Deontay Wilder anayeshikilia ubingwa wa WBC.

Amepangiwa kucheza pambano lake lijalo kwenye uwanja wa Wembley, jijini London Aprili mwakani, ingawa mpinzani bado hajaamuliwa,kati Mmarekani Wilder au Mwingereza mwenzake Tyson Fury.