Maajabu: Tuzo ya Mchezaji Bora wa Mwezi wanaisikia kwa majirani tu

Muktasari:

Ligi Kuu England imekuwa na utaratibu wa kutoa tuzo ya mchezaji bora wa mwezi, kocha bora hiyo ni kutokana na kiwango anachokionyesha mchezaji katika mwezi husika

LONDON, ENGLAND. Ama kweli wakati mwingine maisha huwa hayatendi haki. Kwenye Ligi Kuu England kumeshuhudia mastaa kadhaa wakifanya mambo makubwa na kuwa msaada kwa timu zao, lakini utashangaa kuna orodha hiyo ya wakali nane, kwa uhodari wao wote, kwenye ligi hiyo hawajawahi kushinda tuzo ya mchezaji bora wa mwezi kwenye ligi hiyo.

 

8. David de Gea

Kipa David De Gea amekuwa mchezaji bora wa msimu kwenye kikosi cha Manchester United kwa misimu mitatu mfululizo. Medali za ubingwa wa Ligi Kuu England, Kombe la FA, Kombe la Ligi na Ngao ya Jamii vyote hivyo amebeba sambamba na Europa League. Lakini, utashangaa kwamba De Gea hajawahi kuchaguliwa kuwa mchezaji bora wa mwezi kwenye Ligi Kuu England. Kipa huyo Mhispaniola alitua Old Trafford mwaka 2011 na ameshavuka mechi 300 akiwa na kikosi hicho cha Man United. Katika muda wake aliokuwa katika kikosi hicho ameshinda tuzo za mchezaji bora wa mechi mara sita, Desemba 2017 aliweka rekodi kwenye Ligi Kuu England kwa kuokoa hatari nyingi zilizokaribia kuwa bao kwenye mechi dhidi ya Arsenal. Aliokoa hatari 14, ambazo dhahiri zilikuwa mabao, lakini hiyo haikutosha kumpa kipa huyo tuzo ya mchezaji bora wa mwezi.

 

7. Patrick Vieira

Kiungo huyo matata kabisa kuwahi kutokea kwenye Ligi Kuu England, akicheza soka lake la kiwango cha juu sana akiwa na Arsenal, Vieira hajawahi kuchaguliwa mshindi kwenye tuzo ya mchezaji bora wa mwezi licha ya kwamba huduma yake ilikuwa muhimu sana wakati timu hiyo ilipobeba ubingwa msimu wa 2000/01. Msimu uliofuatia, Vieira alichaguliwa kuwa nahodha wa timu hiyo ya Arsenal na kuingoza timu hiyo kucheza bila ya kupoteza mechi hata moja kwa msimu wa 2003/04 na kubeba ubingwa, huku kiungo huyo akifunga bao la ushindi katika mechi ya mwisho ya msimu dhidi ya Leicester City. Msimu uliofuatia, Vieira ambapo ilikuwa msimu wake wa mwisho kwenye kikosi hicho cha Arsenal, alifunga penalti ya ushindi kwenye Kombe la FA katika mechi dhidi ya mahasimu wao Tottenham na alifunga pia kwenye mechi dhidi ya Liverpool licha ya kwamba timu yake ilipoteza mechi hiyo.

 

6. Vincent Kompany

Mchezaji mwingine matata kabisa kwenye Ligi Kuu England na medali kadhaa za ubingwa wa ligi hiyo, Vincent Kompany, ambaye hajawahi kushinda tuzo ya mchezaji bora wa mwezi hata mara moja. Beki huyo wa kati alikuwa mchezaji muhimu kwenye kikosi cha Manchester City kilichokuwa chini ya Roberto Mancini, ambacho kilibeba ubingwa wa ligi katika msimu wa 2011/12. Katika msimu huo, Mbelgiji huyo alkicheza mechi 31 na kufunga mabao matatu. Alifunga bao pekee lililoamua mechi yao ya Manchester derby iliyofanyika Aprili kwenye mwaka huo waliobeba ubingwa. Kwa kifupi, Kompany alikuwa mchezaji muhimu kwenye kikosi hicho na ilichanganya kuona ameshinda kushinda tuzo hiyo ya mchezaji bora wa mwezi kwenye Ligi Kuu England. Bado anakitumikia kikosi hicho cha Etihad ambacho kwa sasa kipo chini ya kocha Pep Guardiola.

 

5. Peter Schmeichel

Kipa Schmeichel ameshinda ubingwa wa Ligi Kuu England mara tano akiwa na Manchester United na alikuwa mtu muhimu wakati kikosi hicho kilipobeba mataji matatu makubwa ndani ya msimu mmoja, 1998/99. Kipa huyo raia wa Denmark alishinda tuzo ya kuwa mchezaji bora wa msimu wa 1995/96 huko Man United wakati kikosi hicho kilipoipiku Newcastle United ya Kevin Keegan kwenye ubingwa wa ligi.

Akiwa na Aston Villa kipa huyo alipaswa kabisa kushinda tuzo ya mchezaji bora wa mwezi, hasa kwa kiwango alichokionyesha Oktoba 2001. Katika mechi huo, Aston Villa walishinda mechi tatu kati ya nne, mbili hawakuruhusu bao. Kwenye mechi ya kipigo cha 3-2 kutoka kwa Everton inaweza kuwa shida, lakini hapo Schmeichel aliweka rekodi ya kuwa kipa wa kwanza kufunga bao kwenye Ligi Kuu England. Lakini, tuzo ya mwezi huo ilibebwa na Rio Ferdinand, ambapo wakati huo alikuwa na kikosi cha Leeds United.

 

4. Riyad Mahrez

Leicester City walitumia Pauni 400,000 tu kupata huduma ya Riyad Mahrez. Hakika ilikuwa pesa ndogo sana kutumia kwa staa mwenye kiwango bora kama staa huyo. Mahrez alikuwa kwenye ubora mkubwa sana huko Leicester City kwenye msimu wa 2015/16 ambapo aliwasaidia kubeba ubingwa wa Ligi Kuu England katika staili iliyowashangaza wengi. Katika mechi zake 37 kwenye ligi alizocheza msimu huo, winga huyo wa Kialgeria alifunga mabao 17 na kuasisti 11 na alichagulia kuwa mchezaji bora wa mwaka baada ya msimu kumalizika. Lakini, kitu cha ajabu hakuwahi kushinda tuzo yoyote ya mchezaji bora wa mwezi. Mahrez hakuchaguliwa kwenye tuzo hiyo ya mwezi licha ya kwamba kwa Desemba 2015 alifunga mabao sita, ikiwamo hat-trick dhidi ya Swansea City na lile bao lake matata kabisa dhidi ya Chelsea, lakini haikutosha kuchaguliwa kuwa bora kwa mwezi huo na badala yake tuzo alinyakua Odion Ighalo.

 

3. Alexis Sanchez

Sanchez alichaguliwa kuwa mchezaji bora wa mwaka wa PFA akiwa chaguo la mashabiki katika msimu wake wa kwanza kwenye kikosi cha Arsenal. Lakini, kwa kiwango chake bora alichokionyesha kwenye kikosi hicho cha Arsenal kwa muda wote, Sanchez hajawahi kushinda tuzo ya mchezaji bora wa mwezi. Staa huyo wa kimataifa wa Chile alifaidi tu kwa bao lake kushaguliwa kuwa bora kwenye Ligi Kuu England likitajwa kuwa bora kwa mwezi Oktoba 2015, wakati alipofunga bao maridadi kwenye ushindi wa 3-0 iliyopata Arsenal dhidi ya Manchester United. Kwenye mechi hiyo, Sanchez alifunga mabao mawili moja akipiga shuti nje ya boksi na jingine kwa kisigino. Uhodari wake wote huo aliofanya akiwa na Arsenal hajawahi kuchaguliwa kuwa mchezaji bora wa mwezi. Kwa sasa anaichezea Man United.

 

2. Yaya Toure

Kiungo matata zaidi kuwahi kutokea kwenye kikosi cha Manchester City. Alikuwa mchezaji muhimu kwenye kikosi hicho wakati kilipobeba mataji mawili ya Ligi Kuu England, huku Muivory Coast huyo akitajwa kwenye kikosi cha msimu cha PFA katika misimu hiyo miwili ya 2011/12 na 2013/14. Lakini, ushangaa, Yaya Toure hajawahi kushinda tuzo ya mchezaji bora wa mwezi. Staa huyo alifunga bao muhimu kwenye ushindi dhidi ya Newcastle United, Mei 2012 kabla ya bao la Sergio Aguero. Katika msimu wa 2013/14 alifunga mabao 24 katika michuano tofauti. Mabao matano kati ya hayo aliyafunga kwenye mechi Machi, yakijumuisha hat-trick kwenye mechi dhidi ya Fulham, hapo ni baada ya kufunga mabao manne kwa mwezi Septemba na manne mengine Desemba, lakini miezi hiyo yote hakuchaguliwa kuwa bora na tuzo zikanaswa na Aaron Ramsey na Luis Suarez mara mbili.

1.Didier Drogba

Ana medali nne za ubingwa wa Ligi Kuu England akiwa na kikosi cha Chelsea, lakini cha ajabu, Didier Drogba hajawahi kushinda tuzo ya mchezaji bora wa mwezi. Drogba alisaidia Chelsea kushinda ubingwa wa ligi kwa misimu miwili mfululizo walipokuwa na Jose Mourinho katika awamu yake ya kwanza huko Stamford Bridge, kisha akaendelea kutamba kwenye timu hiyo wakati kocha huyo alipoondoka. Muivory Coast huyo alishinda Kiatu cha Dhahabu na mabao yake 20 kwenye msimu wa 2006/07 na alichaguliwa kwenye vikosi bora vya msimu vya PFA, FIFPro na UEFA, huku akiwa wa nne kwenye Ballon d’Or. Msimu wa 2009/10, alikuwa kinara wa mabao wa Ligi Kuu England baada ya kufunga mabao 29 katika mechi 32 alizocheza. Lakini, utashangaa, Drogba hajawahi kushinda tuzo ya mchezaji bora wa mwezi.