Milioni 50 za DP Ruto kuia Ethiopia, Wanyama hana presha

Muktasari:

Harambee Stars, wanakalia usukani mwa kundi F, wakiwa na alama tatu baada ya mechi tatu, sawa na Ethiopia na Ghana, na wanahitaji kushinda mchezo wa leo, kujiongezea matumaini ya kufuzu kombe la Mataifa ya Afrika, itakayopigwa mwakani, nchini Cameroon.

Nairobi, Kenya. Wanasema pesa ni sabuni ya roho. Pesa inaweza kuhamisha milima na kukusanya maji katika utulivu wa hali ya juu. Historia inathibitisha hilo. Vitabu vya dini vinatuambia hivyo. Naibu wa Rais William Ruto anaamini hivyo!

Ni ngumu kuamini kama sio mfuatiliaji wa matukio ya kihistoria. Ni ngumu kuamini kuwa pesa ina nguvu ya kuhamisha milima kama hujawahi kusoma Biblia, lakini ukweli ni kwamba Pesa ilimsukuma Judas Eskariote, kumsaliti Yesu Kristo.

Yule Delilla aliahidiwa pesa, akaamua kusaliti penzi la Samsoni. Kuelekea mechi ya leo kati ya Kenya na Ethiopia, Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Kenya, ameamua kutumia nguvu ya pesa kwa kufuata maandiko, kuwahamasisha Harambee Stars, kuiua Ethiopia, ugani Moi Kasarani.


Kufuatia ukata unaokabili timu hiyo, ambapo taarifa zilieleza kuwa Kocha wa Stars hajalipwa mishahara ya miezi mitatu huku wachezaji nao wakiwa wanadai posho zao, Naibu wa Rais, Dr. William Ruto, alijitokeza jana na kukabidhi Sh25 milioni, kwa ajili ya gharama za maandalizi ya mechi ya leo.

Aidha, Ruto hakuishia hapo, aliahidi kutoa milioni 50, endapo Harambee Stars itafanikiwa kuifunga Ethiopia alasiri ya leo, na kujiweka sawa katika kampeni za kusaka tiketi ya kwenda Cameroon.

“Mwaka jana kama mnakumbuka kuna ahadi tulitoa. Leo nimekuja kuthibitisha hilo. Tuko pamoja katika vita ya kuelekea Cameroon. Tunahitaji ushindi, na Ethiopia akifungwa tu, natoa milioni 50. Swala la marupurupu tumeshalimaliza. Jumapili tukatekeleze wajibu wetu,” alisema DP Ruto.

Wakati huo huo, Nahodha wa Stars, Victor Wanyama amewataka wachezaji kutokuwa na presha, huku akiahidi kufanya awezalo kuhakikisha Ethiopia wanafungwa pale kasarani na kuhitimisha miaka 14 ya kusubiri.

“Kinachotakiwa ni utulivu wa kiakili, tucheze kama timu, tushambulie na kuhakikisha tunaepuka presha ya aina yoyote ile. Najua watakuja wakiwa wamejipanga kutuzuia lakini umoja na mshikamano pamoja na sapoti ya mashabiki ndicho kitakachotusaidia,” alisema Wanyama.