Hawa Diamond akwama Uwanja wa Ndege Dar

Muktasari:

Msanii Hawa wa Diamond na mama yake wamezungumzia sakata la kukataliwa kusafiri kwenda nchini India jana kwa ajili ya matibabu na kueleza kuwa sasa itabidi warudi Muhimbili.

Dar es Salaam. Msanii Hawa Said na mama yake Ndaguna Shabani waliokuwa waondoke jana kwenda nchini India kwa ajili ya matibabu na kushindwa kufanya hivyo wamezungumzia hali hiyo.
Hawa maarufu kwa jina la Hawa wa Diamond ambaye anasumbuliwa na ugonjwa wa ini kwa zaidi ya mwezi sasa, aalikutana na kikwazo hicho baada ya kutokuwa na kibali cha daktari cha kupanda ndege.
Jana ilikuwa wasafiri na ndege ya Shirika Emirate lakini safari hiyo ilikwama wakati wakiwa katika hatua ya kukaguliwa nyaraka zao mbalimbali za kusafiria ndani ya Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere(JNIA).
Wakizungumza na MCL Digital, nyumbani kwao Buguruni muda mfupi baada ya kurejea kutoka uwanja wa ndege kwa sharti la kutopigwa picha, mama Hawa amesema baada ya kukosekana kwa nyaraka ya kibali cha daktari waliambiwa kwamba hata wakiruhusiwa kusafiri wataishia Dubai.
Ndagina amesema jambo hilo kwao ingekuwa ngumu kwani lingewaingiza gharama za kukaa kwenye nchi ya watu bila sababu hivyo njia sahihi ikaonekana bora warudi nyumbani.
Pia alitaja sababu nyingine kwamba ni kutokana na kutokuwa na daktari au nesi wa kuwasindikiza ambapo kama Hawa angepata tatizo lolote akiwa safarini angeweza kumpa msaada.
Hata hivyo amesema kwa sasa kila kitu kuhusu safari hiyo wanamsikilizia Meneja wa Diamond Babu Tale awaambie kuwa itakuwa lini tena kwa kuwa yeye ndio anasimamia kila kitu na wao ni kufuata maelekezo ya nini wanachotakiwa kufuata.
Kwa upande wake Hawa amesema kushindwa huko kusafiri kumemuumiza kwa kuwa bado anaugulia maumivu na kwa wiki nzima alikuwa akiongezeka kuvimba tumbo na miguu.
"Yaani hapa hali ninavyoiona itabidi nirudi muhimbili wakanitoe tena maji katika hospitali ya Muhimbili ambapo wakifanya hivyo maumivu walau hupungua kidogo, kwani sijajua safari tens itakuwa lini mpaka hapo tutakapopata maelekezo mengine" amesema Hawa.


 
  Hawa alifahamika kwenye ulimwengu wa sanaa kupitia wimbo wa 'Nitarejea' ambao Diamond aliomshirikisha. Kwa sasa anasumbuliwa na ugonjwa wa ini amvao unamsababishia kujaa maji tumboni na kuvimba miguu.
 

Kutokana na ugonjwa huo ameshalazwa katika hospitali ya Taifa ya Muhimbili zaidi ya mara nne na kutolewa maji tumboni ambao kuna wakati alikuwa hutolewa hadi lita nne.