Ethiopia wameapa kuiadabisha Kenya, Kasarani

Mesfin Mulualem

Muktasari:

Katika mchezo wa kwanza uliopigwa jijini Addis Ababa, katika dimba la Bahir Dar, siku ya Jumatano, Oktoba 10, mwaka huu, timu hizi mbili zilitoshana baada ya kutoka sare ya 0-0, ambapo mchezo wa leo ni lazima ushindi upatikane, haijalishi nani atashinda kati ya Harambee Stars na Ethiopia.

Nairobi, Kenya. Wahabeshi na kiburi chao kama mnavyowafahamu. Wameapa kuwaliza wakenya katika Ardhi yao, mbele ya mashabiki wao.    Habari ndio hiyo, Ethiopia ambao wametua nchini tayari kwa ajili ya mtanange wa leo, wameapa kutoa kichapo na sio vinginevyo!
Kwa mujibu wa kiungo wao hatari, Mesfin Mulualem, baada ya kulazimishwa sare ya 0-0, ugani Bahir Dar mbele ya mashabiki wao zaidi ya 80,000, wamesafiri hadi Nairobi kwa lengo moja tu, kulipiza kisasi kwa kuiharibia Harambee Stars mbele ya mashabiki 60,000 watakaofurika ugani Moi Kasarani.
"Tuliumizwa sana na ile sare. Hatukutegemea ingekuwa vile. Kila mtu anafahamu hali yetu kwenye msimamo wa kundi ukoje.
"Tunahitaji ushindi kwa njia yoyote ile, leo tutahakikisha tunaondoka na pointi tatu, tumekuja Nairobi kwa ajili hiyo tu,” alisema Mulualem
Licha ya kutamba kuwa wamekuja kupata ushindi, kiungo huyo hakusita kukimwagia sifa kikosi cha Kenya huku akiendelea kusisitiza kuwa baada ya kuwasoma mastaa wa Stars, wana uhakika wa kushinda mchezo wa leo, wakitumia mbinu zilezile walizotumia pale Bahir Dar.
Kimahesabu Ethiopia wapo pabaya hasa baada ya Sierra Leone kufungiwa na Shirikisho la Soka  Afrika (CAF) na sasa wanakalia kuti kavu, wakiwa mkiani mwa msimamo wa Kundi F, linaloongozwa na Kenya. Wanahitaji kushinda mchezo wa leo kivyovyote ile.