Rivaldo ampeleka Hazard kwa Real Madrid

Friday October 12 2018

 

Rio de Janeiro, Brazil. Kiungo nyota wa zamani wa Barcelona na timu ya Taifa ya Brazil, Rivaldo ameitaka Real Madrid kuongeza bidii ya kuisaka saini ya Eden Hazard wa Chelsea.

Rivaldo alisema kuwa hakuna siri kwamba Real itayumbishwa na pengo la Ronaldo na kuwa inapaswa kufanya kila liwezekanalo kumsaka mrithi wake na mtu sahihi kwa sasa atakayeziba pengo hilo ni Hazard.

“Nimemsikia Hazard akitamka kuwa ndoto yake ni kuona siku moja akiichezea Real Madrid, kwa kauli hii ni wazi kuwa mchezaji huyu yupo tayari kujiunga nayo hivyo ni jukumu la Rais wa Real, Florentino Perez kupambana kumsajili najua anaweza,” alisema Rivaldo.

Kiungo huyo aliyeitumikia Barcelona kati ya mwaka 1997–2002 alisema kwamba, anaufahamu vema utamaduni wa kiuchezaji wa Real na kwa jinsi alivyomuona Hazard anaamini atafiti kwenye klabu hiyo.

“Ninadhani Real Madrid wanapaswa kufikiri mara mbili kuhusiana na namna ya kumpata mtu atakayechukua nafasi ya Ronaldo ambaye kila mmoja anajua alikuwa na umuhimu wa aina yake kikosini hivyo kuondoka kwake lazima kutaleta athari kubwa,” alisema na kuongeza.

“Ningekuwa na nafasi ya kuwashauri ningewaambia wamsajili Hazard haraka, kutokana na utamaduni na namna ya uchezaji wao huyu ndiye atakayefiti ni mchezaji wa aina yake na kizuri zaidi ni kwamba mwenyewe amekiri kwamba ana mapenzi makubwa na klabu hiyo, bila shaka atafanya kazi ya ziada kuipa timu mafanikio hivyo ni lazima wamsajili,” alisema.

Alisema alikunwa sana na namna mchezaji huyo alivyoisaidia nchi yake katika fainali za mwaka huu za Kombe la Dunia zilizofanyika nchini Russia kwa Ufaransa kutwaa ubingwa huku Ubelgiji ikishika nafasi ya tatu.

Hata hivyo pamoja na Hazard kusema kwamba anapenda kwenda Real, amethibitisha kuwa ana furaha mpya ndani ya Chelsea na kwamba hataihama klabu hiyo ya Stamford Brdge katika uhamisho ujao wa Januari.

Advertisement