Mashabiki Simba Mwanza wamuombe MO

Muktasari:

Mo ametekwa leo asubuhi akiwa anaelekea kwenye mazoezi katika hoteli ya Colosseum jijini Dar es Salaam.

Mwanza. Wakati hali ya sintofahamu ikiendelea kutanda baada ya kutekwa mfanyabiashara maarufu nchini, Mohamed Dewji 'Mo' na watu wasiojulikana, mashabiki wa soka jijini Mwanza wamesema kwa sasa ni kumwombea apatikane akiwa salama.
Dewji 'Mo' ambaye ni mdhamini wa klabu ya Simba ametekwa na watu wasiojulikana wakati akienda mazoezini mapema leo jijini Dar es Salaam.
Wakizungumza na MCL Digital mashabiki wa soka ambao ni wanachama wa Klabu ya Simba jijini hapa wamesema kwakuwa mamlaka zinaendelea kufanya uchunguzi wa tukio hilo wao wanaendelea kumwombea apatikane akiwa hai.
Salya Ludanha, Hassan Kaheshi na Juma Mlilo wamesema bado ni mapema na vyombo vya dola vinaendelea kufanya kazi yake, wao wanaelekeza nguvu katika maombi ili 'Tajili' huyo aweze kupatikana akiwa salama.
Ludanha ambaye ni Mwenyekiti wa muda wa Klabu ya Simba Mkoa wa Mwanza, amewaomba mashabiki kuwa na subra kwa kipindi hiki.
"Bado ni mapema sana lakini niwaombe mashabiki wa Simba yule ni kiongozi wetu kwahiyo watulie wakati mamlaka zikiendelea kufanya kazi yake" amesema Ludanha.
Naye Kaheshi ambaye ni shabiki wa Simba, amesema kuwa kwa sasa lao ni dua ili aweze kupatikana kigogo huyo akiwa salama.
"Siwezi kuzungumza zaidi kwa sababu ni mapema ni jambo la kusubiri tu, lakini kikubwa ni kuomba dua ili aweze kupatikana akiwa salama" amesema Kaheshi.