Genk, Stars zamfikirisha Samatta mbali

Muktasari:

Samatta amekuwa moja wa wachezaji tegemeo katika kikosi cha Taifa Stars akiwa ni kinara wa kuzifumania nyavu

Praia, Cape Verde: STAA wa klabu ya Genk na timu ya taifa ya Tanzania, Mbwana Samatta anaota kuingia katika orodha ya wachezaji watatu watakaowania tuzo za mwanasoka bora wa Afrika kama akipata mafanikio na timu hizo mbili mwaka huu.
Samatta na Genk wapo vizuri katika michuano ya Europa msimu huu licha ya kufungwa hivi karibuni na Sarpsborg ya Norway kundi L mabao 3-1, pia kwa upande wa Stars, kuna dalili ya kutinga katika michuano ya Afcon kama watamalizia vema mechi za kundi lao.
Sasa Samatta anaamini kama Genk itafika robo fainali ya Europa Ligi huku Stars ikifuzu kwenda Afcon kuna uwezekano mkubwa akafikiriwa kutinga hatua ya wachezaji watatu wanaowania tuzo za Afrika.
“Wakati mwingine huwa najihesabia kwamba nina bahati. Kuna uwezekano mkubwa nikawekwa katika orodha ya wachezaji bora wanaowania tuzo za Afrika kama Genk itafika mbali katika michuano ya Europa huku nikiiwezesha Stars kutinga michuano ya Mataifa ya Africa.” alisema Samatta.
Samatta anaamini kwamba kitendo cha kuchaguliwa kama mwanasoka bora wa ndani barani Afrika katika miaka ya karibuni kimemuwezesha kwa kiasi kikubwa kuangaliwa kwa karibu na watu ambao wanaandaa tuzo hizo.