Zawadi ya bingwa wa Ligi Kuu Zenji yatua ZFA

Muktasari:

  • Vifaa vilivyotolewa na Kampuni hiyo ni Kombe kubwa, Medali 30 za Dhahabu, Medali 30 za Fedha huku wakiahidi kutoa Jezi, Mipira, Vifaa vyengine vya michezo pamoja na fedha taslim kwa ajili ya zawadi za bingwa na makamu bingwa wa ligi hiyo.

Zanzibar. Chama cha Soka Visiwani Zanzibar (ZFA) kimepokea zawadi za mabingwa wa ligi kuu Soka ya Zanzibar kwa msimu wa mwaka 2017-2018.

Zawadi ambazo zinatarajiwa kutolewa rasmi Oktoba 18, 2018 kwenye mchezo wa Ngao ya Jamii utakaochezwa kati ya Bingwa wa ligi kuu ya Zanzibar ambao ni JKU dhidi ya bingwa wa Kombe la FA ambae bado hajapatikana.

Akikabidhi zawadi hizo Afisa Uhusiano wa Kampuni ya ZAT Ali Juma (Ali Raza) amesema kutokana na kuguswa na Michezo wameona ipo haja kusaidia zawadi hizo kwa Bingwa na Makamu Bingwa wa ligi kuu ya Zanzibar.

Amewaomba wadau wengine wasaidie Michezo ili kuendana na kasi ya Maendeleo ya Michezo  inayofanywa na  Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk Ali Mohamed Shein.

Kwa upande wake Katibu wa Kamati ya Mashindano kutoka ZFA Alawi Haidar Foum amesema zawadi hizo zitatumiwa kama zilivyokusudiwa huku akiwaomba wadau wa Soka kufata vyema kalenda ya ZFA ili kuendana na wakati.

Akitoa Shukrani Mwenyekiti wa Kamati ya Mashindano ya ZFA Hussein Ali Ahmada amewapongeza kampuni ya ZAT kwa kusaidia Michezo Zanzibar huku akiwaomba wadau wengine kujitokeza kusaidia ZFA kwani bado ina wakati mgumu kwaajili ya kuendesha shughuli hizo za Soka.