Bao la kwanza lampa jeuri straika Geita Gold Sports

Muktasari:

Straika huyo alishawahi kuwa mfungaji Bora katika msimu wa 2015/16 wa Ligi Daraja la Kwanza  kwa kufunga mabao 17 wakati alipokuwa kwenye kikosi hicho cha Geita Gold Sports na msimu huu anajipanga kila mechi kutupia mabao.

BAADA ya kufunga bao lake la kwanza kwenye Ligi Daraja la Kwanza msimu huu Straika wa Geita Gold Sports,Omary Kanyoro amesema kwake kazi ndio imeanza kwani amepata mzuka na sasa kila mechi atakayocheza lazima atupie nyavuni.

Straika huyo wa zamani wa Stand United alifunga bao la ushindi katika mchezo wao na Maafande wa Polisi Tanzania uliopigwa uwanja wa Waja mkoani humu ambapo Geita Gold Sports ilishinda bao 1-0.

Akizungumza na Mwanaspoti,Mshambuliaji Kanyoro alisema bao hilo limeweza kumpa mzuka wa kupambana kwenye Ligi hiyo ambapo sasa kila mechi atakayocheza lazima atupie.

“Lile bao ni kama limefungua njia kwangu kuanzia sasa nitapambana kila mechi niweze kutupia kwani nataka niwe mfungaji bora kama nilivyofanya kwenye msimu wa 2015/16 ambapo nilifunga mabao 17”alisema Kanyoro.

Alisema yeye ni mzoefu wa Ligi Daraja la Kwanza hivyo anajua ugumu wake lakini atapambana kuhakikisha Geita Gold Sports inafanya vyema na kupanda Ligi Kuu msimu ujao.

“Ligi Daraja la Kwanza ina ugumu wake kuliko mashindano mengine ni lazima upambane kweli kweli hivyo nitapambana kwa kushirikiana na wenzangu kuweza kuipandisha Ligi Kuu Geita Gold sports ”alisema Straika huyo.

Hata hivyo Straika huyo aliwataka mashabiki wa soka wa mkoa wa Geita kuipa sapoti kubwa timu hiyo katika safari hiyo ya kuipeleka kwa mara ya kwanza Ligi Kuu.

Geita Gold Sports ipo kwenye kundi B ambapo mpaka sasa ina pointi Nne baada ya kucheza mechi mbili wakiwa nafasi ya pili kwenye msimamo wakiongozwa na Arusha United kwenye pointi Nne wakitofautiana mabao ya kufunga na kufungwa.