Penati ya Mahrez yaibua mengine

Muktasari:

Riyad Mahrez ameweka rekodi ya kukosa penalti tano kati ya nane alizopiga hivi karibuni huku akiwanyima ushindi muhimu Manchester City dhidi ya Liverpool uwanjani Anfield.

LIVERPOOL, ENGLAND. NUSURA Manchester City iondoke na pointi zote tatu pale Anfield juzi Jumapili usiku kama Pep Guardiola angekuwa anaijua rekodi ya upigaji penalti ya staa wake wa kimataifa wa Algeria, Riyad Mahrez. Kumbe alikuwa hajui.
City ilipata penalti katika dakika ya 85 ya pambano hilo na Gabriel Jesus alitaka kupiga penalti hiyo lakini akapokea maagizo kutoka kwa Guardiola kuwa Mahrez ndiye aliyetakiwa kuuweka nyavuni mpira huo.
Matokeo yake Mahrez alibutua mpira juu ya lango la kipa wa Liverpool, Alisson Becker na pambano hilo kumalizika kwa suluhu ya bila ya kufungana. Na sasa wapekuzi wa mambo wamemlaumu Guardiola kwa kumpa penalti hiyo Mahrez.
Imebainika Mahrez ana rekodi mbovu katika upigaji wa penalti ambapo amekosa penalti tano kati ya nane za mwisho alizopiga. Penalti ya mwisho aliyokosa ni ile alipokuwa Leicester City dhidi ya Manchester City Mei 2017.
Na sasa Guardiola amekiri  alikuwa haijui rekodi mbovu ya penalti inayomwandama Mahrez huku akimuomba msamaha Jesus kwa kumzuia kupiga penalti hiyo huku mpigaji namba moja, Sergio Aguero akiwa ameshatolewa uwanjani.
“Mahrez alikuwa na moyo wa kupiga penalti dakika zile. Katika mazoezi huwa anapiga vizuri sana. Mwisho wa siku mambo kama haya yanatokea. Mwisho wa siku ndivyo kama ilivyokuwa,” alisema kocha huyo Mhispaniola.
“Wakati wa mazoezi kila siku namuona Mahrez akipiga penalti na ilinifanya nijiamini. Litakuwa funzo kubwa kwake (kukosa penalti), siku nyingine mpira utaingia wavuni. Jesus alitaka kupiga lakini namuomba msamaha. Yalikuwa maamuzi yangu,” aliongeza Guardiola.
Alipobanwa zaidi aliongeza kwa kusema: “Mpigaji wa siku zote, Sergio hakuwepo uwanjani, lakini mara nyingi tunafanyia mazoezi penalti. Tulikuwa na nafasi ya dakika za mwisho kushinda mechi lakini tumekosa. Tutajaribu kufanya vema siku za mbele,” alisema Guardiola.
“Kwa kawaida kwa miezi sita, saba iliyopita penalti zote alikuwa anapiga Sergio lakini saa zile alikuwa katika benchi. Alikuwa uwanjani wakati tuliponyimwa penalti ya kwanza. Labda tulihitaji penalti mbili kwa ajili ya kufunga bao moja. Nisingependa kuongelea kuhusu waamuzi, au kuhusu maamuzi. Tuongelee kuhusu mechi. Soka,” aliongeza Guardiola.
Penalti ya Liverpool ilisababishwa na beki staa wa kimataifa wa Uholanzi, Virgil Van Dijk, ambaye alikosea katika ukabaji na kujikuta akimkwatua nyota wa kimataifa wa Ujerumani, Leeroy Sane aliyeingia kipindi cha pili kuchukua nafasi ya Raheem Sterling.
Van Dijk ambaye amekuwa akisumbuliwa na mbavu, amekiri hakuwa na matatizo na penalti hiyo na alikubali moja kwa moja maamuzi ya Mwamuzi, Martin Atkinson.
“Haukuwa uamuzi mzuri kupiga ‘tackling’ pale. Ilikuwa ni penalti. Nilimwambia mwamuzi pia, ilipaswa kuwa, lakini ni wazi hatukufungwa. Niliitazama ilivyopigwa kwa sababu nilikuwa nataka kuwahi kuokoa katika mpira ungerudi ndani. Nina furaha haukuingia,” alisema Van Dijk.
“Nadhani walifanya vema, tulifanya vema, mpaka ilipotokea penalti. Ilikuwa mechi nzuri kucheza, bahati mbaya hatukufunga, bahati nzuri hatukuruhusu bao pia,” aliongeza beki huyo ambaye ni ghali zaidi duniani baada ya kununuliwa kwa dau la Pauni 75 milioni kutoka Southampton Januari mwaka huu.
Kwa sasa ligi itasimama kupisha wikiendi ya mechi za kimataifa na ikirudi Oktoba 20, Manchester City itakuwa nyumbani kukabiliana na Burnley wakati Liverpool itakuwa ugenini kukabiliana na Hudderslfied Town.