Diamond Platinumz ametufundisha hili kwa vitendo zaidi

Muktasari:

Mwanatandale hata kama leo anaishi maisha ya kisupa staa, lakini hajasahau alikotoka. Juzi alirudi Tandale kivingine akiwaandalia shoo ya kibabe wanatandale wenzake kama sehemu ya maadhimisho ya siku yake ya kuzaliwa, kisha kurejesha shukrani kwa jamii.

Staa huyo ametumia zaidi ya Sh 80 milioni kwa ajili ya kugawa bodaboda 20 kwa Vijana wa Tandale, kugawa mtaji wa kati ya Sh100,000-200,000 kwa akinamama 100 na kuwakatia bima ya Afya wakazi 1000 mbali na kugawa matanki ya maji katika shule nne na kuikarabati moja aliyosomea.

NI kweli huwezi kupendwa na wote, hata uwe mtu mwema kiasi gani. Kadhalika huwezi kuchukuliwa hata uwe katili na hayawani wa kiasi gani! Ndivyo maisha yalivyo. Binadamu kaumbwa na silika ya kumchukia ama kumpenda mtu wakati mwingine bila sababu.

Binadamu wanajua kutoa hila na vilevile wanajua kuficha udhaifu wa mtu kwa vile tu anampenda ama kumchukia.

Hata hivyo kuna wakati nafsi husuta. Wahenga waliwahi kusema mnyonge mnyongeni, lakini haki yake mpeni. Juzi Ijumaa, mitaa ya Tandale. Mitaa inayochukuliwa kama moja ya sehemu duni za watu kuishi. Uswahilini sana kama ilivyo Mwananyamala, Kigogo, Buguruni, Mburahati ama Tandika. Mitaa hiyo ni mitaa fulani iliyojaa usela na vituko vya aina yake, huku mazingira yake yakiwa ya kipekee kulinganisha na maeneo mengine. Duniani kote maeneo kama hayo yapo, sio jijini Dar es Salaam tu ama Tanzania pekee.

Mitaa hiyo ndiko alikozaliwa na kukulia na hata kutoka kimuziki kwa Staa wa sasa wa muziki wa kizazi kipya. Ndio, Diamond Platinumz. Hajivungi, anajivunia kuwa

Mwanatandale hata kama leo anaishi maisha ya kisupa staa, lakini hajasahau alikotoka.

Juzi alirudi Tandale kivingine akiwaandalia shoo ya kibabe wanatandale wenzake kama sehemu ya maadhimisho ya siku yake ya kuzaliwa, kisha kurejesha shukrani kwa jamii.

Staa huyo ametumia zaidi ya Sh 80 milioni kwa ajili ya kugawa bodaboda 20 kwa Vijana wa Tandale, kugawa mtaji wa kati ya Sh100,000-200,000 kwa akinamama 100 na kuwakatia bima ya Afya wakazi 1000 mbali na kugawa matanki ya maji katika shule nne na kuikarabati moja aliyosomea. Hili lilikuwan somo kubwa kama masomo mengine ambayo Diamond amekuwa akiwasomesha wenzake kwa vitendo tangu alipoibuka mwaka 2009 mpaka leo akiwa mmoja wa mastaa wakubwa nchi na duniani kwa ujumla.

Alitoa somo la kujituma ili mtu afanikiwe. Kujichanganya anga la kimataifa kuteka soko la dunia, achilia mbali kuwaacha mbali aliwakuta ama alioanza nao kwa kuwa na menejimenti ya kijanja na inayojua dunia ya kisasa inataka nini kimuziki.

Nirejee tukio lake la Tandale. Kwa hakika alichokifanya wala sio kitu kidogo. Ni jambo la kusisimua na kumtofautisha staa huyo na wauza sura wengine ambao katika maadhimisho ya siku zao za kuzaliwa, huishia kula bata wenyewe na kuposti picha ya jinsi walivyochezea noti..! Hakuna anayepangiwa cha kufanya, ila Diamond katoa somo!

Bahati mbaya ni kwamba hasidi hana sababu, kwani tayari kuna walioibuka na kuhoji kwanini iwe Tandale na sio kwingineko, huku wale ambao mara nyingi wamekuwa wa kwanza kumkosoa Diamond, wakipatwa na kwikwi na kushindwa kusema lolote.

Mitandao ilipoa mno kwa juzi tofauti na zile posti zilizokuwa zikimcharura staa huyo alipovaa kipini, alivyovaa kikukuu ama kusuka nywele ama juzi kati alipotoa msaada kwa Hawa Diamond anayeugua...Binadamu hana hila na hana shukrani kama tumbo! Tumbo ukishiba ni tamu, likiwa na njaa ni balaa...mbaya ni kwamba hata likilishwa bado halishukuru!

Ukweli ni kwamba Diamond hawezi kuwa msanii wa kwanza nchini kurudisha shukrani kwa jamii, lakini kitendo chake cha kukumbuka alikotoka na kuyagusa makundi tofauti katika kuwainua kiuchumi ni mfano wa kuigwa.

Hata kama hajawaridhisha wote kwa kile alichokitoa, lakini bado anastahili pongezi kwa sababu angeweza kufuata mkumbo wa mastaa wengine kuchezea fedha waliozovuna kupitia wanajamii na mwishowe kuzitupia tu picha za bata lake kuwarusha roho watu!

Ndio, maana narejea kusema, hili linaweza kuonekana ni jambo dogo sana na pengine kudhaniwa labda Diamond kataka kutengeneza kiki kwa malengo yake, lakini ukweli jambo lake limegusa mioyo ya wengi na mastaa wengine wajifunze kupitia kwake.