WAMETISHA: Wameanza kuliamsha dude mapema tu ligi kuu

Beno Kakolanya

Muktasari:

Ligi Kuu Bara iliendelea kwenye viwanja mbalimbali nchini na baadhi ya wachezaji nyota waliendelea pia kung’ara. Kakolanya atakumbukwa zaidi mchango wake pale alipokosekana katika mchezo wao na Stand United, licha ya kushinda lakini ilifungwa mabao mengi (matatu) na hapo langoni alisimama Klaus Kindoki.

WAKATI Ligi Kuu Bara ikiendelea huku baadhi ya timu zikikaribia raundi ya 10, wapo nyota ambao wameng’ara mapema na kuziwezesha timu zao kuwa katika nafasi nzuri kwenye msimamo wa ligi.

Wikiendi hii, Ligi Kuu Bara iliendelea kwenye viwanja mbalimbali nchini na baadhi ya wachezaji nyota waliendelea pia kung’ara. Mwanaspoti linakuletea nyota ambao wameng’ara kwenye mechi zao za kwanza hadi sasa.

Eliud Ambokile - Mbeya City

Ni mshambuliaji anayekuja kwa kasi ingawa hata msimu uliopita aliipambania timu yake huku akiwa ni mfungaji bora wa timu hiyo.

Hadi jana Jumamosi kabla ya mechi za jioni ndiye aliyekuwa anaongoza kwa idadi kubwa ya mabao.

Amethibitisha ubora wake baada ya kufunga mabao sita na kumwacha mbali Mfungaji Bora wa msimu uliopita Emanuel Okwi ambaye hadi sasa hajafunga bao hata moja katika mechi alizocheza. Okwi alifunga mabao 20.

Amekuwa mcheza mchezaji bora wa mwezi Septemba huku akizua gumzo kwa wadau wa soka nchini kukosekana kuitwa kwenye kikosi cha timu ya Taifa ‘Taifa Stars’ ambacho kinajiandaa na mechi dhidi ya Cape Verde kujiandaa kufuzu AFCON.

Meddie Kagere - Simba

Amesajiliwa na Simba msimu huu akitokea Gor Mahia ya Kenya baada ya kuonyesha kiwango safi kwa mabingwa hao wa ligi ya KPL.

Amekuwa katika kikosi cha kwanza cha Kocha Mbelgiji Patrick Aussems, amecheza karibu mechi zote za ligi huku akifunga mabao manne.

Mnyarwanda huyu amekuwa kipenzi cha mashabiki wa Wekundu kutokana na mchango na huenda mambo yakamnyookea huko mbele na kuwa miongoni mwa nyota wanaowania kiatu cha dhahabu msimu huu.

Hashim Mussa na Said Khamis-Mbao FC

Licha ya wachezaji wa Mbao kwa jumla wamepambana kila mmoja kwa uwezo wake lakini mafanikio ya klabu hiyo yamechagizwa sana na nyota hao wawili.

Kipa Hashim Mussa amekuwa ni msaada mkubwa ndani ya kikosi hicho chini ya Kocha Amri Said ‘Stam’ kwani kati ya mechi nane walizocheza ameruhusu mabao matatu pekee.

Said Khamis amefunga mabao matatu hadi sasa na amekuwa msaada mkubwa kwenye timu hiyo kwa kusaidiana na mzoefu Pastory Athanas katika safu ya ushambuliaji na kwa jumla wamefikisha mabao sita.

Razack Abarola na Tafadzwa Kutinyu –

Azam FC

Hadi sasa Azam imeshuka dimbani mara saba na kukusanya pointi 15 na inashika nafasi ya pili kwenye msimamo lakini kipa wao Abarola ameruhusu bao moja tu.

Pamoja na timu hiyo kuwa na kikosi kizuri na Benchi la Ufundi chini ya Kocha Hans Pluijm, Abarola amekuwa na msaada mkubwa pale langoni kwa kusimama vyema kuokoa hatari zote.

Mbali na Abarola, Kutinyu naye amekuwa moto kwenye timu hiyo kutokana na kuisaidia klabu yake kuifungia mabao matatu kati ya saba yaliyofungwa.

Ile kasi yake aliyotoka nayo Singida United bado anaendelea nayo na lolote linaweza kutokea huko mbele kama atazitumia vyema nafasi anazopata katika ufungaji mabao.

Alex Kitenge na Bigirimana Blaise -Stand United

Alex Kitenge ni raia wa Burundi na ni mara yake ya kwanza kucheza soka nchini, amekuwa na mwanzo mzuri baada ya kusaidia timu yake kuifungia mabao matatu.

Moto wa Kitenge uliwaka zaidi katika mechi yao na Yanga akiibuka kidedea baada ya kufunga hat-trick na kuweka rekodi mpya msimu huu.

Kuna kisu kingine Blaise ambaye tayari katupia mabao matatu na kuwa kati ya wachezaji 10 ambao wamefunga idadi kubwa ya mabao.

Blaise ambaye ni msimu wake wa pili akiwa ndani ya kikosi hicho cha wapiga debe, kiwango chake kimeendelea kuwa juu kutokana na msimu uliopita kuisaidia timu yake kufikia Nusu Fainali ya kombe la Shirikisho.

Stamili Mbonde -

Mtibwa Sugar

Mshambuliaji huyu licha ya kushindwa katika vita ya kuwania tuzo ya mchezaji bora mwezi uliopita, lakini amekuwa na mchango mkubwa katika timu yake baada ya kuifungia mabao manne. Mbonde amedumu Mtibwa Sugar zaidi ya msimu mmoja amekuwa na mchango mkubwa wa kukusanya pointi 16 zilizoiweka Mtibwa kileleni mwa ligi.

Kwa namna alivyoanza iwapo hatapata kashkashi yoyote kama majeraha au kadi nyekundu anaweza kubeba hata tuzo ya mfungaji bora au mchezaji bora miezi ijayo.

Habib Kyombo -Singida United

Straika huyu tayari wamefunga mabao matatu kati ya saba ambayo timu hiyo imefunga, huku akionekana kuwa na kasi yake kama msimu uliopita akiwa Mbao FC.

Kyombo ambaye msimu uliopita aliing’arisha Mbao FC kwa kufunga mabao 15 yakiwamo sita ya Kombe la Shirikisho (FA) na kutwaa tuzo ya mfungaji bora wa michuano hiyo, huenda neema ikamwangukia tena msimu huu akiwa na uzi mpya.

Ibrahim Ajibu na Beno Kakolanya-Yanga

Mshambuliaji Ibrahim Ajibu licha ya kuwa na bao moja hadi sasa lakini amekuwa mhimili wa Yanga kwani kati ya mabao tisa waliyofunga ameshiriki kwa asilimia kubwa.

Hadi sasa Ajibu ana asisti nne ambazo zimesaidia timu yake kuwa katika nafasi ya nne ikiwa na pointi 13 huku wakiwa wamecheza mechi chache kuliko timu yoyote. Eneo la golini limekamatwa na Beo Kakolanya ambaye amekuwa mkali na hiyo ilithibitika zaidi katika mechi yao na watani zao Simba kwa namna alivyookoa hatari nyingi.

Kakolanya atakumbukwa zaidi mchango wake pale alipokosekana katika mchezo wao na Stand United, licha ya kushinda lakini ilifungwa mabao mengi (matatu) na hapo langoni alisimama Klaus Kindoki.