NO AGENDA: Alikichofanya DIAMOND PLATNUMZ kimenikumbusha WARREN BUFFETT

Sunday October 7 2018

 

By Luqman Maloto

MWAKA 2007 (miaka 11 iliyopita), nilisoma jarida la Forbes. Mahojiano mazuri na tajiri mwenye mawe mengi, Warren Buffett. Kipindi hicho, Buffett alikuwa tajiri namba mbili duniani, nyuma ya Bill Gates. Niliandika makala gazetini mwaka huo kwa kutafsiri mahojiano hayo.

Wakati huo, Buffett alikuwa ametoa fedha nyingi kuchangia mfuko wa Gates na mkewe, Melinda Gates, unaoitwa Bill & Melinda Foundation, ambao hujishughulisha na ustawi wa maisha ya watoto, vijana, watu wenye kuishi katika mazingira magumu, waathirika wa Ukimwi na makundi mengine yenye uhitaji.

Buffett aliulizwa na waandishi wa Forbes; inakuwaje yeye ambaye ni tajiri namba mbili amchangie fedha tajiri namba moja? Alijibu: “Ni ujinga kufikiri namchangia Bill. Mimi nachangia mfuko na lengo ni kuhakikisha makundi kusudiwa yanapokea misaada. Kila mmoja anapaswa kuchangia kulingana na uwezo wake.”

Jawabu la Buffett lilimaanisha kuwa si kwa sababu Gates ni tajiri namba moja ndiyo aachiwe peke yake mfuko wake wa kusaidia jamii. Bali, kila mmoja kwa nafasi yake anatakiwa kuona umuhimu wa kusaidia. Kinachofurahisha ni kuwa mwaka uliofuata, Forbes walimtangaza Buffett kuwa tajiri namba moja duniani. Gates akawa wa pili.

Hapo unaupata ukweli kutoa si kujitia umaskini. Hekima ndani ya methali ya Kiswahili chetu ni ‘Kutoa ni moyo usambe ni utajiri’. Hata sasa, Buffett akiwa tajiri namba tatu duniani nyuma ya Jeff Bezos na Gates, bado ni mchangiaji mkubwa katika mfuko wa Bill na Melinda.

Msimamo wake ni, utajiri wake wote na kila senti itakayokuwa inatengenezwa na taasisi yake ya Berkshire Hathaway baada ya yeye kufariki dunia, vitatumika kutoa misaada. Kwamba watoto wake hawatarithi chochote. Maana amewatosheleza kiuchumi wakiwa hai.

Ana watoto watatu tu, wa mwisho ana umri wa miaka 60, mwingine miaka 63 na mkubwa miaka 65. Wote ni matajiri. Huo ndiyo mpango wa Buffett ili wasiguse mali zake akifa, kusudi zitumike kusaidia jamii yenye uhitaji duniani. Anataka kila mwenye nacho kidogo atoe.

MWITE CHIBU BUFFETT

Diamond Platnumz hujiita Dangote. Akijipa ubatizo wa kitajiri kupitia tajiri namba moja Afrika, Aliko Dangote. Kwa vile jina lake kwenye hati ya kusafiria ni Nasibu Abdu Juma, basi akataka aitwe Chibu Dangote. Hata hivyo, jina Simba ndilo limemkaa sana.

Juzi (Ijumaa), Diamond alifanya kitu ambacho wengi hawafanyi. Kwa kutazama tabia za utoaji na kusaidia watu, alizonazo Buffett, unaachaje kumfananisha Diamond na Buffett? Kwa nini iwe Chibu Dangote na isiwe Chibu Buffett?

Oktoba 2, mwaka huu, Chibu alitimiza miaka 29. Chibu alikulia Tandale, Dar es Salaam. Juzi (Oktoba 5), aliamua kufanya tukio ambalo linamfanya kuwa mmoja wa Watanzania wenye mioyo mikubwa ya kutoa sehemu ya walichonacho ili kusaidia jamii pana.

Muhimu zaidi, alidhihirisha ni kwa kiasi gani maisha yake ya muziki, biashara na mafanikio kwa jumla, yalivyo na athari chanya kwa jamii ya Kitanzania. Kuna watu wana pesa nyingi kuliko Diamond, lakini hazina mchango wenye kugusa jamii moja kwa moja.

Diamond aliwezesha kina mama 1,000 Tandale kupata bima ya afya. Akawapa mitaji kinamama 100 wa Tandale. Kuna vijana Tandale wamepewa bodaboda. Alifanya ukarabati wa shule Tandale na kadhalika. Leo, wanawake hao, wakiumwa hawahangaiki gharama za matibabu. Kwa mwaka mzima watatibiwa bure.

Tafakari ukubwa wa jambo alilofanya. Matibabu bure. Kinamama kwa mitaji waliopewa na vijana bodaboda walizopewa, hao wamepewa maisha. Mizunguko ya biashara watakazofanya, zitajenga maisha yao binafsi, zitakuza ajira, zitasisimua mzunguko wa kifedha na zitachangia Pato la Ndani la Taifa (GDP). Kuna mlemavu alipewa bajaji na kadhalika.

Wangapi wamewahi kufanya kama Diamond? Kina nani wana fedha nyingi na wameziatamia mithili ya kuku kwa mayai yake au vifaranga vyake? Kitendo cha kuamua kusherehekea kuzaliwa kwake kwa kuwajengea uwezo wa kiuchumi wengine pamoja na bima za afya, huko ndiko kurejesha kwa jamii (giving back to society).

Kurudisha kwa jamii ndiyo hulka ya Buffett. Pengine Diamond angeweza kudhani wanaofaa kutoa ni mabilionea kama Said Bakhresa, Mohammed Dewji, Reginald Mengi na wengine, kwa hiyo angesema akae asubiri awe tajiri kama wao ndipo atoe, ila ameona mbona alichonacho anaweza kuwagawia na wengine? Ametoa. Kwa nini nisimwite Chibu Buffett?

DIAMOND KATOA DARASA

Si Darassa wa Maisha na Muziki, namaanisha Diamond ametoa bonge ya shule. Kwa kinamama waliopata bima za afya, mitaji, vijana waliopewa bodaboda, ukarabati wa shule uliofanywa, aliyepewa bajaji na kila kilichofanyika, kinatoa somo la hali ya juu.

Somo kwa wasanii; kazi yao inaweza kujenga au kustawisha maisha ya wengi kwenye jamii. Yaani pamoja na ajira za moja kwa moja kutokana na mauzo au vipato vya kazi zao, wao wenyewe, kwa ushawishi na masalio yao ya kifedha benki, wanaweza kuzipa mguso chanya jamii zao.

Somo hili linahusu wasanii wengine kujitathamini, kuona uwezo wao. Wasisubiri mpaka wawe na uwezo kama Dewji, Mengi au Bakhresa, maana Diamond angesubiri afike huko asingeigusa jamii kwa namna ambavyo ameweza kufanya hivi sasa. Wakumbuke kutoa ni moyo.

Darasa lingine kwa wasanii ni kujituma. Hakuna kificho Diamond anafanya kazi kwa bidii kubwa. Mafanikio yake yanaakisi juhudi zake. Hivyo, ni wito kwa wasanii wengine kupambana ili milango mingi zaidi ya riziki ifunguke. Jinsi itakavyofunguka, ndivyo watakavyoigusa jamii kwa upana zaidi.

Lipo somo kwa wafanyabiashara, maofisa watendaji wakuu kwenye taasisi binafsi za kibiashara, wabunge na mawaziri. Wajiulize Diamond ameweza vipi? Je, wao hawana cha kurejesha kwenye jamii? Unadhani Diamond kila alichofanya kimetoka kwenye akaunti zake benki? Yapo maeneo alitumia ushawishi.

Wabunge wajiulize; wao hawana ushawishi kwenye taasisi za kifedha au watu binafsi wenye uwezo ili kusaidia miradi yao ya kusaidia jamii za majimbo yao? Mawaziri je? Wafanyabiashara kwa kiwango cha vipato vyao nao wajitathimini. Wanasema mbuzi hula kwa urefu wa kamba yake. Buffett anasema kila mtu lazima atoe. Ni somo kubwa kwa Serikali na mifumo yake. Mamlaka zitambue kuwa sanaa ni ajira inayoweza kuleta matokeo makubwa kwenye jamii. Diamond amefanya alichoweza. Jiulize kama Tanzania ingekuwa na wasanii 100 wenye uwezo na moyo kama Diamond. Jamii ya Kitanzania ingeponywa kiasi gani?

Siyo kumtazama Diamond na kukenua, ifahamike Diamond amefanikisha aliyofanikisha kwa sababu ana pesa. Pesa zake ni matokeo ya mafanikio aliyonayo. Diamond angekuwa mwanamuziki maskini, yeye mwenyewe angekuwa mzigo, hivyo asingemudu kumsaidia yeyote. Watu waliopo kwenye mamlaka za Serikali, wabadilike. Watumie akili na ubunifu wao kusaidia kukuza sanaa na kuwawezesha wasanii kuwa na njia rahisi za kufanikiwa.

Siyo kuwabana na makato mengi mpaka wanafeli. Wakifeli tutawapataje kina Diamond wengi? Mwisho kila mtu kwa nafasi yake atoe. Jitahidi kugusa maisha ya mtu japo mmoja. Huo ndiyo u-Diamond, huo ndiyo u-Buffett.

Advertisement