MOURINHO AKATWE TU!

Muktasari:

Man United hawana sababu ya kuwaza sana itakuwa vipi kama watamtimua Mourinho, kwa sababu kuna makocha wengine kibao, wasiopungua 10, ambao wanaweza kuwachukua na kuja kubadilisha kabisa upepo na kuweka mambo sawa huko Old Trafford.

MANCHESTER, ENGLAND. MABOSI wa Manchester United wanalazimika kukanusha taarifa kibao zinazohusu kumfuta kazi Jose Mourinho zilizokuwa zikizagaa kwenye mitandano ya kijamii wikiendi hii. Kulikuwa na ripoti zikidai kwamba Mourinho atafutwa tu kazi bila ya kujali atakuwa ameshinda mechi dhidi ya Newcastle United au la. Lakini, wanasema hivi, lisemwalo lipo kama halipo, basi li njiani laja!

Hata hivyo, Man United hawana sababu ya kuwaza sana itakuwa vipi kama watamtimua Mourinho, kwa sababu kuna makocha wengine kibao, wasiopungua 10, ambao wanaweza kuwachukua na kuja kubadilisha kabisa upepo na kuweka mambo sawa huko Old Trafford.

Zinedine Zidane

Kitu kizuri kuhusu Zidane ni kwamba ni gwiji kwenye mchezo wa soka. Ameucheza kwa mafanikio na hata alipokuja kuwa kocha, ameifanya kazi hiyo kwa mafanikio makubwa, akibeba mataji matatu ya Ligi ya Mabingwa Ulaya mfululizo mbele ya macho ya makocha wengine mahiri kama Mourinho mwenyewe na Pep Guardiola. Shida pekee inayomkabili ni kwamba hana uzoefu wa Ligi Kuu England na Man United atakayokuja kuinoa si sawa na ilivyokuwa Real Madrid.

Mauricio Pochettino

Mashabiki wa Man United wangependa sana kuona Pochettino anakuwa kwenye benchi lao. Kitu kinachowafurahisha kuhusu kocha huyo ni kwamba anacheza soka lenye mvuto na kisha amefanya mambo makubwa kwenye kikosi cha Tottenham Hotspur licha ya kuwa na bajeti finyu kwenye usajili. Akienda Old Trafford atampata mchezaji anayemtaka, hivyo kuna uwezekano akaonyesha makali yake makubwa sana. Tatizo pekee la Pochettino ni kwamba hajawahi kushinda taji lolote.

Laurent Blanc

Ni kocha mzoefu wa kubeba mataji baada ya kubeba taji la Ligi Kuu Ufaransa akiwa na Bordeaux kabla ya kwenda kupata mafanikio makubwa kwenye kikosi cha Paris Saint-Germain. Aliwahi kuichezea Man United, hivyo atakuwa anafahamu utamaduni wa timu hiyo kwa kiasi fulani. Blanc ni mchezaji ambaye hata wachezaji wenyewe watamheshimu kwa sababu ya utaratibu wake, hazibizani na wachezaji mambo yasiyokuwa na maana. Shida inayomkabili kocha huyo ni kwamba amefanya kazi Ufaransa tu na amekuwa bila ya kazi ya ukocha kwa zaidi ya miaka miwili sasa.

Michael Carrrick

Ni kocha msaidizi kwenye kikosi cha Man United kwa sasa. Jambo zuri kuhusu Carrick ni kwamba ni gwiji wa klabu hiyo na amecheza kwa mafanikio makubwa akijitengenezea jina kubwa linaloheshimika na kila mchezaji kwenye timu. Kitu pekee kinachotia wasiwasi kwenye kumbadili kocha mwenye uzoefu kama Mourinho, Carrick bado hajakuwa kocha mzoefu, licha ya kuelezwa kwamba amekuwa na kipaji kikubwa. Lakini, suala la kupewa nafasi ndio la msingi kwa sababu hata mbuyu ulianza kama mchicha.

Brendan Rodgers

Ni kocha anayehusudu kucheza soka lenye kuvutia. Hakika, Rodgers mpira wake unavutia sana, amelifanya hilo Swansea, Liverpool na sasa yupo na Celtic. Kitu ambacho kitawafanya Man United kumfikiria Rodgers mara mbili na pengine wasimpe ajira ni kwamba alikuwa kwenye timu mahasimu wao, Liverpool na huko hakuwa amefanya vizuri licha ya kwamba alikaribia kabisa kubeba ubingwa wa Ligi Kuu England kama si nahodha wa Anfield kwa wakati huo, Steven Gerrard kufanya makosa ambayo yalichangia pia timu kupoteza nafasi hiyo ya kubeba ubingwa wao wa kwanza wa Ligi Kuu.

Antonio Conte

Anapatikana tu, hana kazi kwa sasa tangu alipofutwa kazi huko Chelsea mwishoni mwa msimu uliopita. Conte ni kocha wa kiushindi, mara nyingi amekuwa akifikiria kushinda tu na ndio maana amepata mafanikio Juventus na kwenye kikosi cha Chelsea, akibeba ubingwa wa Ligi Kuu England katika msimu wake wa kwanza tu kabla ya kufutwa kazi huko Stamford Bridge. Shida inayomkabili Conte haina tofauti na Mourinho, amekuwa mpenzi wa kucheza soka la kukaba kitu ambacho ni rahisi kutibuana na wachezaji pindi anapoona kwamba hawafanyi kitu anachotaka kifanyike.

Leonardo Jardim

Amefanya maajabu makubwa huko kwenye kikosi cha AS Monaco tangu alipowasili hapo mwaka 2014, akiwaibua wachezaji vijana na kuibana PSG katika ubingwa wa Ligi Kuu Ufaransa, hivyo Monaco kuibuka mabingwa mwaka jana. Maajabu yake yaliendelea hadi kwenye Ligi ya Mabingwa Ulaya, ambapo kikosi hicho kilikwenda hadi kwenye hatua ya nusu fainali. Amewahi kuzinoa pia klabu kubwa Ureno na Ugiriki. Shida kubwa ni kwamba hajawahi kunoa timu kwenye Ligi Kuu England huko Monaco yake ni timu ndogo haiwezi kulingana na presha ya kuwa kocha wa Man United.

Max Allegri

Mara kadhaa, Allegri amehusishwa na klabu za Ligi Kuu England kwa miaka ya karibuni baada ya kufanya vyema kwenye kikosi cha Juventus alikobeba mataji ya Serie A mara nne mfululizo huku akifika fainali ya Ligi ya Mabingwa Ulaya mara mbili. Huko nyuma aliwahi kushinda pia ubingwa wa Serie A akiwa na AC Milan pia. Ni kocha wa daraja la juu na ndiye aliyemtumia Paul Pogba kwa mafanikio makubwa hadi Man United kutoa pesa ndefu kumsajili tena mchezaji huyo. Tatizo lililopo ni kwamba hajawahi kufanya kazi nje ya Italia, huku Juventus hawaonekani kama watakubali kumpoteza kocha wake kwa sababu uwepo wake kwenye timu hiyo ulichangia pia kwa kiasi kikubwa kwa Cristiano Ronaldo kuchagua kujiunga na wababe hao wa Turin.

Ryan Giggs

Ni mchezaji mahiri zaidi kuwahi kutokea kwenye kikosi cha Man United wakati wa enzi zake alipokuwa akicheza. Kwa sasa Giggs ni kocha wa timu ya taifa ya Wales. Alishawahi kuwa kocha wa Man United, wakati alipochaguliwa kama kocha mchezaji chini ya David Moyes kabla ya kuchaguliwa kuwa kocha msaidizi timu hiyo ilikuwa chini ya Louis van Gaal. Lakini, Moyes alipoondolewa kwenye timu, Giggs alikuwa kocha wa muda hadi Van Gaal alipokuja kuchukua mikoba. Ameondoka Man United baada ya Mourinho kutua na watu wake. Tatizo ni kwamba ana timu tano tu alizoinoa Wales, hivyo bado hajawa kocha mwenye uzoefu mkubwa huku itakuwa ngumu kuachana na kazi ambayo ndiyo kwanza ameteuliwa, huku dhamira yake ikiwa kuifikisha Wales kwenye michuano ya Euro 2020.

Roberto Martinez

Martinez yupo juu baada ya kuisaidia Ubelgiji kushika nafasi ya tatu kwenye fainali za Kombe la Dunia 2018, huku timu ikicheza soka lenye mvuto mkubwa. Alifanya mambo makubwa pia alipokuwa Wigan, ambapo aliwapa ubingwa wa Kombe la FA, huku timu yake ikicheza soka maridadi. Aliwahi kuinoa pia Everton kwenye Ligi Kuu England. Shida kubwa ya Martinez ni moja tu, timu yake huo haikabi. Timu inacheza vizuri, soka la kuvutia, lakini shida inakuja kwenye kuzuia.