Simba yaokoa mamilioni

Muktasari:

KWA muda mrefu Simba imekuwa ikihaha kusaka viwanja vya kufanyia mazoezi, huku ikitumia kiasi kikubwa cha fedha kwa msimu mmoja, lakini kwa kuanza ukarabati wa uwanja wake wa mazoezi ina maana klabu itaokoa zaidi ya Sh 40 milioni.

SIMBA wajanja sana. Ingawa imewachukua miaka 10 kabla ya kuanza kuujenga uwanja wao wa mazoezi eneo la Bunju, lakini kukamilika kwa uwanja huo kutaifanya klabu hiyo kuokoa zaidi ya Sh 40 milioni msimu huu.

Kiasi hicho cha fedha ni kile ambacho Simba ingetumia kama gharama ya kukodi viwanja kwa ajili ya kufanyia mazoezi katika kipindi cha miezi minne ya mwisho katika msimu wa Ligi Kuu 2018/2019.

Tangu kuanzishwa kwake Simba haikuwahi kuwa na uwanja wake wa kuchezea mechi, ingawa miaka kadhaa nyuma walikuwa na wa kufanyia mazoezi eneo la Jangwani kabla ya serikali kuweka mradi ya malori.

Lakini unaambiwa baada ya kiwanja cha Jangwani kubinafsishwa, klabu hiyo imekuwa ikitangatanga kabla ya mwaka 2010 waliponunua uwanja huo, hivyo kuifanya iwe inatumia zaidi ya Sh 10 milioni kila mwezi kwa ajili ya kukodi viwanja vya mazoezi kujiandaa na mechi za mashindano mbalimbali inayoshiriki.

Ukubwa wa gharama ya fedha hizo unatokana na kiwango cha ada ambayo Simba hutozwa na wamiliki wa viwanja vya Boko Veteran na Gymkhana Club ambavyo imekuwa ikivitumia kufanyia mazoezi yake.

Pindi inapofanyia mazoezi katika Uwanja wa Boko Veteran ambao upo maeneo ya Boko nje kidogo ya jiji la Dar es Salaam jirani kabisa na fukwe ya Bahari ya Hindi, Simba hulipia Sh 300,000 ili kufanya mazoezi kwenye uwanja huo kwa muda wa saa mbili na nusu tu.

Lakini pale ambapo benchi lake la ufundi linapendekeza timu hiyo ikafanye mazoezi yake kwenye Uwanja wa Gymkhana uliopo Posta jijini pia jirani na fukwe wa Bahari ya Hindi hulazimika kulipia Sh 500,000 kwa ajili ya kufanya mazoezi kwa muda wa saa mbili tu.

Kwa wastani, Simba imekuwa ikifanya mazoezi siku tano kwa wiki jambo linaloifanya itumie takribani kiasi cha zaidi ya Sh 2.5 milioni kwani mara nyingine hufanya mazoezi kwa awamu mbili asubuhi na jioni hasa kwenye Uwanja wa Boko Veteran.

Gharama hiyo ya Sh 2.5 milioni ambayo Simba inatumia kwa ajili ya kulipia viwanja vya mazoezi kwa wiki, maana yake ikijumlishwa kwa mwezi ambao una wiki nne, inafikia kiasi cha Sh 10 milioni na kwa miezi 12, jumla ni Sh 120 milioni.

Kwa mujibu wa Mwekezaji Mkuu wa Simba, Mohammed Dewji, ujenzi wa uwanja huo wa Bunju utakamilika na kuanza kutumika kabla ya Februari, 2019. Maana yake ni kwamba Simba itaokoa kiasi cha Sh 40 milioni ambazo ingetumia kukodisha viwanja katika kipindi cha miezi Februari, Machi, Aprili na Mei kabla msimu haujafungwa. Hivi karibuni Kamati ya Leseni za Klabu ya TFF ilizichimba mkwara Simba na Yanga kwa kutotimiza kanuni klabu za Ligi kwa kuwa na viwanja.