Klabu nchini ziache kulalamika, zinapaswa zijitathimini kwanza

Muktasari:

Ni kweli kuna baadhi ya waamuzi hufanya maamuzi ya ajabu uwanjani, lakini bado klabu zinastahili kubeba lawama kwa matokeo yao mabovu uwanjani badala ya kukimbilia kuwanyooshea vidole wengine.

IMEKUWA ni mazoea kwa miaka ya karibuni, kila baada ya mechi iwe ni katika Ligi Kuu Bara ama Ligi Daraja la Kwanza au Daraja la Pili na hata michuano mingine yoyote kusikia malalamiko.

Kuanzia kwa wasemaji wa klabu, makocha, viongozi mpaka hata wachezaji na mashabiki kila mmoja huwa hakosi lawama dhidi ya waamuzi wa mechi zao ama kulia na ubovu wa viwanja.

Lawama zimekuwa zikitoka kwenye timu kubwa mpaka zile za ndogo bila kujali madaraja wanayocheza, ilimradi kila mmoja asikike akilalamika. Ni nadra kusikia wadau wa klabu zinazoshiriki ligi hizo kuweza kutoa kauli za kuridhika na matokeo hata kama wanajua wamefungwa kihalali.

Ukisikia wadau wa klabu wakisifia matokeo yao na kuwapongeza waamuzi, basi usisumbuke kujiuliza kwani lazima timu zao zimeshinda. Ni mara chache kusikia maofisa habari, makocha ama hata manahodha wa timu sambamba na viongozi, wanachama na mashabiki klabu za hapa nchini kukiri kupoteza mchezo kwa makosa yao.

Lawama kwenye soka imekuwa ni kama utamaduni fulani na umechangia kwa kiasi kikubwa kuwalemaza wachezaji wakiamini wanapoteza mechi zao kwa kuonewa, kufanyiwa hujuma na hata kufanyia vitendo vya kishirikina.

Hawapendi kukubali katika soka kuna suala la kuzidiwa maarifa uwanjani, hivyo kuchangia kupoteza mechi ama kupata matokeo yasiyotarajiwa. Soka ni mchezo wa hadharani na ni mchezo ambao timu moja ikifanya kosa lazima iadhibiwe. Hiyo ndio raha ya soka. Kocha Jose Mourinho na klabu yake ya Man United unadhani wamafurahishwa na vipigo vya mara kwa mara wanavyopewa katika Ligi Kuu ya England? Hapana! Lakini wanamezea na kubeba maumivu yao kimyakimya kwa kutambua makosa yao uwanjani ndio yanayowagharimu.

Jambo hilo linapaswa pia kuzingatiwa na klabu za Tanzania, soka ni mchezo wa makosa na daima huwa na matokeo matatu yasiyokwepeka, kufunga, kufungwa ama kupata sare.

Lakini kwa sababu klabu zetu kupitia wadau wake, huwa hawapendi kuonekana wazembe wanapopata matokeo mabovu, hutafuta chaka la kujificha ndio maana wao huwa wanalalamika tu hata pasipostahili kulalama. Kwa hali kama hiyo, Mwanaspoti linadhani imefika wakati sasa klabu kupitia wadau wake kuanza kuijitathimini katika kila mechi wanazocheza ili kubaini kama matokeo mabovu wanayopata ni makosa yao kisha kujipanga upya.

Klabu zinalalamikia ubovu wa viwanja, sawa ni kweli viwanja vinavyotumiwa kwa mechi za ligi zote nchini ni aibu kwani ni vichache tu vyenye hadhi na ubora unaotakiwa, lakini je klabu zinazolalamika zenyewe zinamiliki viwanja?

Asilimia kubwa hazina viwanja hata vya mazoezi, hivyo zinapokuwa zikilalamikia ubovu wa viwanja kuchangia kuzipa matokeo mabaya uwanjani ni kisingizio kisicho na mashiko kwani wenye haki ya kutoa malalamiko kama hayo ni klabu chache tu zenye kumiliki viwanja vya kisasa na vyenye hadhi. Kuhusu suala la waamuzi, hilo limekuwa kama chaka la klabu kila zinapofanya vibaya, ilihali ki undani, huwa zinapata matokeo mabaya kwa sababu timu zao ni dhaifu, hazina mbinu uwanjani na zinaishi kwa mazoea tu.

Kuna baadhi ya timu hazina vikosi vipana, hazina safu nzuri ya mabeki, viungo na hata ushambuliaji na zinapokutana na timu zilizokamilika na kufungwa, mara moja hukimbilia kusingizia waamuzi kuwahujumu ilihali huwa sio kweli.

Kwa hali hiyo ni vyema klabu kupitia viongozi, makocha na wadau wengine kufanya tathmini za vikosi vya timu zao kila zinapocheza kubaini udhaifu wao badala ya kukimbilia kulaumu wasiohusika na matokeo mabaya ya timu zao.

Haiwezekani wachezaji hawajitumi uwanjani kutokana na kutolipwa mishahara ama posho zao kwa muda mrefu, hawajaandaliwa kimwili na kiakili kwa ajili ya mchezo husika, halafu ikifungwa watupiwe lawama waamuzi. Huu ni uonevu.

Ni kweli kuna baadhi ya waamuzi hufanya maamuzi ya ajabu uwanjani, lakini bado klabu zinastahili kubeba lawama kwa matokeo yao mabovu uwanjani badala ya kukimbilia kuwanyooshea vidole wengine.

Hayo yakifanyika, tunaamini kusingekuwa na lawama za kila mara kama ambavyo imekuwa ikishuhudiwa sasa kiasi cha kuchangia kutokea kwa vurugu zinazofanywa na wachezaji dhidi ya waamuzi kwa madai ya kufanyiwa hujuma.