Figisu za Simba zambeba Yondani

Muktasari:

Nyota wa zamani wa Simba na Yanga, Nurdin Bakari amemzungumzia Kelvin Yondan kuwa mfano wa kuigwa na chipukizi kutokana na staili yake alioishi na klabu hizo kongwe.

KELVIN Yondani amekuwa mchezaji tegemeo na anayeheshimiwa mno ndani ya Yanga, lakini imeelezwa kuwa kama sio figisu alizokutana nazo Msimbazi huenda asingepata heshima aliyonayo sasa Jangwani na nchi nzima.

Kiungo kiraka aliyewahi kucheza pamoja na Yondani, Nurdin Bakari ndiye aliyefichua siri hiyo akisema figisu zilizomfanya Yondani aondoke Simba mwaka 2012 na kujiunga Yanga ndizo zilizomfanya awe alivyo sasa akiwa tegemeo kwa klabu na timu ya taifa.

“Mchezaji anapohama moja ya klabu kongwe Simba na Yanga, basi anatakiwa kuwa na akili ya ukomavu kama Yondani, la sivyo inaweza ikamshushia thamani na kutoweka kwenye ramani ya soka. “Nakumbuka Yondani ilifikia kipindi akiwa Simba alipitia magumu mengi na figisu nyingi ambazo zilimfanya afanye maamuzi ya kwenda upande wa pili, Yanga wamekuwa wajanja wa kuendana na maisha anayotaka beki huyo na ndio maana ameendelea kuwafanyia kazi kwa ustadi,” alisema Nurdin aliyekipiga timu zote kwa nyakati tofauti.

Nurdin anayecheza soka Visiwani Zanzibar kwa sasa alisema Yondani amekuwa mfano wa kuigwa soka kama kazi na kuficha mapenzi ya kuonyesha yupo upande gani.

Aidha Nurdin aliyesababisha Tanzania ikafungiwa kwenye michuano ya Vijana U-17 kwa miaka mitatu kuanzia mwaka 2004 baada ya kubainika kuwa na umri mkubwa wakati Serengeti Boys ikifuzu fainali za Afrika U-17, aliwageukia nyota na ishu ya kucheza Ulaya.

Alisema sio kila anayeichezea Simba, Yanga ama Azam anaweza kwenda nje ya nchi kama hazingatii nidhamu na kujituma, kwa vikle soka la kulipwa lina adabu na miiko yake.

“Unajua kwa sasa tofauti na nyakati zetu, tulibaniwa na viongozi wetu ambao walikuwa wanataja dau kubwa ya kuwakatisha tamaa wale wanaotuhitaji, ila kipindi hiki milango ipo wazi tatizo linakuja wengi hawajatokea Akademiki hivyo hawajui wao ni kinanani.”

“Nje wanaangalia vitu vingi sana ambavyo wachezaji wa Tanzania hawana, walio na nafasi ya kufanikiwa kucheza Ulaya ni wale ambao wanatokea kwenye vituo vya soka ila kwa sasa sijaona naona ni siasa tu,” alisema.