Lukaku na rekodi nyingine Ubelgiji

Wednesday September 12 2018

 

 Reykjavík, Iceland. Mshambuliaji Romelu Lukaku jana Jumanne alikuwa shujaa wa Ubelgiji alipofunga mabao mawili na kusababisha penalti iliyozaa bao la kwanza katika ushindi wa mabao 3-0 dhidi ya Iceland.

Huo ulikuwa mchezo wa kwanza kwao wa mashindano ya ‘Euro Nations League’, ambapo Ubelgiji iliyotwaa nafasi ya tatu katika fainali za Kombe la Dunia 2018, imejizolea pointi tatu muhimu, lakini ipo nafasi ya pili katika kundi lake nyuma ya Uswisi ambayo iliibamiza Iceland mabao 6-0.

Ubelgiji ilipata bao la kuongoza lililofungwa na Eden Hazard dakika ya 29 kwa mkwaju wa penalti iliyotokana na Lukaku kuangushwa ndani ya eneo la hatari na Sverrir Ingi Ingason wa Iceland.

Bao la pili lilifungwa dakika ya 31 na Lukaku na kuipeleka nchi yake mapumziko ikiongoza kwa mabao 2-0. Mshambuliaji huyo wa Manchester United aliifungia tena Ubelgiji bao la tatu na la pili kwake dakika ya 81.

Hicho kilikuwa kipigo cha kwanza kwa Iceland nyumbani kwao baada ya kutopoteza katika mechi 13 za michuano mbali mbali ingawa kimekuwa cha pili mfululizo kwenye mashindano mapya ya Nations League kwani ilipoteza mchezo wa kwanza Jumamosi iliyopita ilipofungwa mabao 6-0 na Uswisi.

Advertisement