Harambee Stars kutumia uwanja wa Kasarani

Nairobi, Kenya. Hatimaye timu ya taifa Harambee Stars, itacheza mechi yake ya kwanza katika Uwanja wa Taifa wa Moi Kasarani, baada ya miaka miwili kufuatia uwanja huo kufungwa kupisha ukarabati.

Septemba 8, mwaka huu, kikosi cha Kenya kinachonolewa na Mfaransa Sebastien Migne kitagusa nyasi za Moi Kasarani, ambao ni uwanja rasmi wa wa nyumbani wa timu ya taifa, wenye uwezo wa kuingiza mashabiki wapatao 60, 000, kukipiga dhidi ya Ghana, katika mechi ya kusaka tiketi ya kufuzu Kombe la mataifa ya Afrika, yanayotarajiwa kufanyika mwakani huko Cameroon (2019 AFCON).

Mwaka 2016, Shirikisho la soka  nchini liliutangaza uwanja huo kuwa uwanja wa nyumbani wa timu zote za taifa za Kenya, lakini mwaka mmoja baadae ukafungwa pamoja na ule Nyayo kwa ajili ya matengenezo na sasa limefunguliwa rasmi kwa ajili ya michezo mbalimbali, ukiwemo mchezo wa soka.

Stars ilitarajiwa kurejea katika uwanja huo, mapema mwezi Mei, katika mchezo wa kwanza wa Kocha Migne kama mkufunzi wa timu ya taifa, lakini mchezo huo ukalazimika kuhamishiwa kwenye dimba la Kenyatta, mjini Machakos kwa ajili ya kumalizia ukarabati.

 

Itakumbukwa kwamba, mara ya mwisho, Stars walicheza katika dimba hilo, wakiwa chini ya ukufunzi wa Stanley Okumbi (Novemba 2016), dhidi ya Liberia, wakishinda 1-0. Pia itakumbukwa kuwa, katika kipindi hicho, Stars hawakuwahi kupoteza mchezo hata mmoja wakiwa ugani Kasarani.

Harambee Stars, iliingia dimbani mara tano, ambapo walishinda mara tatu na kutoa sare mbili. Kuanzia kufungulia kwake, dimba hilo, limetumika kuandaa mechi tatu za kimataifa zilizohusisha mabingwa watetezi wa KPL, klabu ya Gor Mahia dhidi ya Hull City ya Uingereza, USM Algiers ya Algeria na Yanga ya Tanzania.

Aidha, uwanja huo umetumika kuandaa michezo miwili ya KPL zote zikiwa ni Derby, mechi ya mashemeji Derby kati ya AFC Leopards na Gor Mahia pamoja na ile ya Slum Derby, kati ya Mathare United na Kariobangi Sharks.

Vijana wa kocha Migne, wataingia katika mchezo huo wa Septemba 8, wakiwa na matumaini ya kufanya vizuri baada ya kuanza vibaya ambapo walilimwa na Sierra Leone huku wapinzanjmi wao Ghana wao wakianza kwa kishindo baada ya kuitungua Ethiopia 5-0.

Mtanange huo utakuwa ni kibarua kigumu kwa Migne na Kikosi chake hasa ikizingatiwa kuwa, Ghana wamewahi kupoteza mara moja tu katika mechi za AFCON tangu mwaka  2009 (walifungwa na Uganda 4-2 mwaka 2014).

 

 

MECHI TANO ZA MWISHO ZA STARS UGANI KASARANI

 

Harambee Stars 1-1 Tanzania

 

Harambee Stars 1-1 Sudam

 

Harambee Stars 2-1 Congo

 

Harambee Stars 1-0 Mozambique 

 

Harambee Stars 1-0 Liberia