VIDEO: KING MAJUTO NI TAFSIRI YA UTAMU NA UKATILI WA SANAA TANZANIA

UNAHITAJI kujua kuwa sanaa ya Tanzania ni tamu? Kioo chako ni uhusika wa fundi Amri Athuman 'King Majuto' alivyokuwa akiwajibika kazini. Na kama unataka uthibitisho kwamba, sanaa ya Tanzania ni katili basi jibu lako ni maisha ya King Majuto.
Naam, King Majuto anakufanya uonje ladha tamu ya sanaa ya Tanzania kwa sababu alikuwa msanii aliyekamilika kwa kiwango cha juu cha ukamilifu. Alitoa huduma bora kwenye tasnia. Na kwa hisani ya teknolojia, huduma hiyo ya King Majuto itaendelea kutufikia hata sasa akiwa ameshalala ndani ya tumbo la ardhi.
Asante teknolojia, King Majuto akiwa ndani ya tumbo la ardhi, kwenye nyumba inayoitwa kaburi, palipo na kizimba kiitwacho mwanandani, sanaa yake itawafikia vitukuu, vinying'inya, vilembwe, vilembwekeze mpaka vitojo, kama ambavyo dunia inaendelea kuhudumiwa na gwiji Charlie Chaplin.
Jina kamili ni Charles Spencer Chaplin, ulimwengu wa sanaa unamtambua kama Charlie Chaplin. Ni heshima kumwita Sir Charlie Chaplin au Sir Charles Chaplin kwa sababu ni mtunukiwa wa tuzo ya heshima ya Ufalme wa Uingereza (Royal Knighthood). Chaplin ni Muingereza na alifariki dunia mwaka 1977 akiwa na umri wa miaka 88.
Alikuwa hodari hasa wa filamu za kuchekesha bila kuzungumza (silent film). Huu ni mwaka wa 41 tangu alipoaga dunia, lakini dunia inaendelea kufaidi ufundi na utundu wake. Mitandaoni, video za Chaplin zina watazamaji wengi mno. Kuna kazi mpya nyingi, lakini zinazidiwa watazamaji na za Chaplin alizorekodi kabla ya mwaka 1960.
Hayo ni matunda ya teknolojia. Hata kazi za King Majuto zinaweza kuwachekesha wajukuu wa wajukuu zetu ikiwa zitatunzwa. Nina hakika kwamba vitojo wetu watatuonea gere tulioishi na kumwona King Majuto kwa macho, ila hawatapata upungufu wa vituko vyake kazini kama ambavyo dunia ya sasa inamfaidi Chaplin.
Dunia ya kijima katikati ya Karne ya 19 ambayo ndiyo hasa Chaplin alikuwa kwenye kilele chake cha umaarufu, watu wengi walioishi zama hizo waliipa kisogo dunia wakiwa hawajui mabalaa yaliyokuwa yakitendwa na Chaplin kwa wakati wao, ni tofauti na sasa. Unaweza kutenda kibweka Kazuramimba, Kigoma, kisha dunia nzima ikakishuhudia.
Laiti Chaplin angeishi katika ulimwengu wa kidigitali kama huu ambao, unatawaliwa na intaneti, bila shaka angekuwa binadamu maarufu kuliko yeyote yule Karne ya 19. Angekufa akiwa tajiri mara 50 zaidi ya utajiri aliouacha.
Huu pia ni mwongozo kwa familia ya King Majuto, kwamba inawezekana mkongwe huyo wa filamu akabaki mashuhuri kwa miaka mingi ijayo kutokana na uamuzi ambao watauchukua. Watumie teknolojia kuenzi kipaji na umahiri wake, vilevile watengeneze fedha.
UTAMU WA SANAA
King Majuto ni kielelezo cha sanaa tamu na bora. Alikuwa hodari wa kufikisha ujumbe na elimu mahsusi kwa njia yenye kutesa mbavu za watu. Kila mzungumza lugha ya Kiswahili, aliyepata kumshuhudia akifanya vitu vyake, hakuacha kukiri kuwa mzee huyo alikuwa na ustadi wa kiwango cha peke yake.
Watu wengi huibeza sanaa ya Tanzania. Huona kama wasanii wake hawaitendei haki. Husimanga kazi zao. Imekuwa sababu siku hizi jina "Bongo Movie" kwa tafsiri ya sinema za kibongo, kuzungumzwa au kutajwa kama kioja cha jamii isiyotambua misingi ya kazi. Bongo Movie inaonekana ni jamii ya watu wanaofanyafanya tu ilimradi kazi ziingie sokoni.
Hata hivyo, nyakati ambazo Bongo Movie wakionekana wababaishaji, King Majuto aliweza kutetea heshima yake katikati ya masimango yaliyoelekezwa kwenye jamii ya sanaa za maigizo nchini. Alibaki na thamani yake. Ni kwa sababu alipokuwa kazini alifanya kile ambacho kingetosha kumvunja mbavu yeyote.
Na huu ndiyo ukweli kwamba, King Majuto amekuwa nembo ya utamu wa sanaa Tanzania tangu analogia mpaka digitali. Chukua aina zote za sanaa, Majuto anateka hadhi ya kutambulika kama kioo cha sanaa ya Tanzania, mbele ya wanamuziki pamoja na makundi mengine ya kisanii.
Wasanii mbalimbali walioanza sanaa kipindi King Majuto anaanza au waliofuata baada yake, hakuna aliyebaki kileleni kama yeye. Baadhi walitangulia kwa wito wa Mungu na waliobaki walififia. King Majuto alibaki kwenye mstari wa juu mpaka kifo kilipomchukua. Hakuwahi kuchoka wala kuporomoka. Alistahili kweli kuitwa King, yaani Mfalme.
Vijana wengi waliingia kwenye sanaa na kumkuta King Majuto, lakini hawakuweza kumtikisa. Waliishia kufanya sanaa ya kiwango chao na kumwacha Mfalme mwenyewe akitikisa kwa kutenda kile alichokiweza kwa umahiri mkubwa. Vijana wengi waling'ara na kufifia lakini jina la King Majuto halikuwahi kupoteza nuru.
Inawezekana King Majuto alitamani kuacha sanaa muda mrefu uliopita, lakini nani angemkubalia? Waandaaji, mapromota na wasambazaji walijua mahitaji ya Watanzania sokoni. Huduma ya King Majuto ilitakiwa mno, ndiyo maana safari za kumfuata Tanga nyumbani kwake ili kumpeleka sehemu za kurekodia filamu, hazikuwa zikikatika.
Tunao wasanii wengi wazuri, lakini hawapati kazi mpaka wanasahaulika. King Majuto alikuwa wa aina yake. Utamu wa sanaa yake tangu miaka ya 1970 mpaka anaingia kaburini, hakuwahi kupoteza ladha, mashabiki hawakutaka kuachana naye, soko nalo lilifanya kila njia ili kufunga naye pingu za maisha.
Akiwa kijana alitikisa kwenye sanaa za maonesho majukwaani. Watu walilia alipoamua kuwaliza na waliteseka kwa kushikilia mbavu alipowachekesha. Akawa miongoni mwa wasanii wa mwanzo kufanya filamu zilizouzwa kwa mikanda ya video (VHF) miaka ya 1990. Na akaenda sawa na kizazi kipya. Mungu amemchukua akiwa bado kileleni.
Vizazi vingi tu vya sanaa vilimkuta King Majuto na kumwacha akipokea kizazi kimoja hadi kingine kilichofuata. Hata kazi alizoacha, zipo nyingi na zitaendelea kutengenezwa mpya baada yake, lakini hazitafua dafu kwa utamu wa sanaa ulioachwa na Mfalme. Kiukweli, King Majuto alikuwa kichuguu sana. Kichuguu kisichochimbika.
UKATILI WA SANAA
Kama sanaa ya Tanzania ingekuwa na roho nzuri, basi King Majuto angekuwa mmoja wa wasanii matajiri Afrika. Miaka zaidi ya 40 yupo kwenye kilele cha biashara ya sanaa, lakini ilipofika wakati wa matibabu ikaanza kuitishwa michango mpaka Rais Dk. John Magufuli alipookoa jahazi.
Ukatili wa sanaa ya Tanzania ni wa kimfumo. Na juu kabisa ikubalike kuwa fedha inayopatikana ni ndogo sana kuliko ambavyo inatakiwa kuwa. Bahati mbaya hili halishughulikiwi, badala yake mamlaka za nchi zinaendelea kukamua hata kidogo chenye kupatikana na kusababisha wasanii wazidi kuumia kuliko kupata ahueni.
Unafuata ubinafsi. Kila mmoja kwenye tasnia anajipendelea kwa kupata zaidi kuliko wengine. Mtayarishaji anawapunja wasanii. Promota na msambazaji naye anataka apate kikubwa zaidi. Mwisho kuna wezi ambao nao wanakuwa na mbinu kali kuhakikisha wanatengeneza fedha nyingi kwa jasho, maarifa na uvumilivu wa wengine.
Inapotokea Bodi ya Filamu na Baraza la Sanaa la Taifa (Basata), wanaibuka na tozo za aina mbalimbali kwenye kazi za sanaa, nalo ni sehemu ya ubinafsi, kwamba taasisi hizo zinaona bora ziwakamue wasanii wenye kumenyeka kuiweka hai sanaa ili wao wapate kile wanachotaka, kisha wasanii waendelee kuwa taabani.
Ulimbukeni wa Watanzania ni sehemu kubwa ya tatizo. Kwanza hawanunui kazi za wasanii, lakini wanaongoza kwa kelele kushambulia kazi zinazoingizwa sokoni. Hata makosa kidogo yenye kuonekana, basi hukuzwa ili kuionesha jamii kwamba Bongo Movie hakuna kizuri chenye kufanyika. Wakati sanaa inakuzwa na teknolojia, wangenunua kazi, pengine fedha zingepatikana za kuboresha kazi. Wataboresha vipi kazi na fedha hawapati?
Yote hayo ukiyaweka kwenye kapu moja, unakuta sanaa ya Tanzania ni katili mno. Kutangatanga kwa King Majuto kupata matibabu ni sawa tu na alivyokuwa swahibu wake, Said Ngamba 'Mzee Small'. Pamoja na nyumba tatu alizojenga na magari aliyomiliki, King Majuto hakuishi maisha yenye thamani ya kazi yake. Na huo ndiyo ukatili wa sanaa ya Tanzania. Ukatili mkubwa mno.