Mziki wa Simba wamshtusha Mkongo

Friday August 10 2018

 

By KHATIMU NAHEKA

KIKOSI cha Yanga, kipo mjini hapa kikijifua, lakini waliifuatilia mechi ya watani wao, Simba walipocheza na Asante Kotoko ya Ghana katika Tamasha la Simba Day na ghafla katika mazoezi ya jana asubuhi Kocha Mwinyi Zahera akawaongezea dozi.
Kocha huyo Mkongo aliamua kuitumia mechi hiyo ya Waghana na Simba kuongeza dozi ya mazoezi kwa wachezaji wake, kwa ni ya kutaka vijana waive vyema kabla ya kurejea kwenye Ligi Kuu Bara kugawa dozi za kutosha kwa wapinzani wao.
Ipo hivi. Kocha Zahera ni mjanja sana, katika tizi la jana aliwakimbiza wachezaji wake kwa mbio za maana walizotakiwa kufika kila kituo cha nusu uwanja kwa kutumia sekunde tano tu kisha kupumzika kwa sekunde 20 kila kituo kimoja.
Vijana wake walipokimbia kama mara tano hivi walionekana kama wanaanza kupunguza kasi na hapo ndipo jamaa akatumia akili ya kujiongeza.
Kocha huyo  aliamua kuwaambia kwa kusema; "Sikilizeni mmeiona ile Asante Kotoko ambayo jana (juzi) imecheza na jamaa zetu na kutoa sare ya 1-1 basi ile mimi niliipiga nne pale Lubumbashi wakapoteana kabisa."
"Hii niliifanya wakati nikiwa na AS Vita Club sasa kama jana (juzi) wametoa sare basi tulieni fanyeni ninachowaambia mtaona faida yake."
Maneno hayo yakawa ni kama yamewaongezea mzuka wachezaji wake ambapo jamaa walianza kuongeza kasi ya maana huku kocha huyo akiwapongeza.
Katika mazoezi ya jana asubuhi wachezaji hao waligusa mpira mara mbili tu, lakini asilimia 96 zilitawaliwa kwa mazoezi ya mbio za kasi na mazoezi makali ya viungo.
Hawakucheza mpira baada ya mazoezi hayo wakaomba dua na kurudi hotelini kwa mapumziko mafupi kabla ya kuendelea na ratiba ya jioni.

Advertisement