Ajibu apewa dozi ya Wawa

BENCHI la Ufundi la Yanga, linafahamu wazi kule kwa watani wao wa Simba kuna beki kisiki, Pascal Wawa na mabeki wengine katili ambao kuwapita lazima straika awe fiti kwelikweli.  Ni sawa tu na ilivyo kwa Azam FC yenye mtu asiyepitika kirahisi kama Aggrey Morris, ndipo kwa kutumia ujuzi wao wakaamua kumpa dozi straika wao, aliyechelewa kambi ya mjini hapa, Ibrahim Ajibu.
Ajibu ametua rasmi kambini na kuungana na wenzake, lakini kana kwamba makocha wake walimpania, jana asubuhi kwenye mazoezi ya timu hiyo walioamua kumpa dozi nene ili kuwekwa fiti kuweza kuhimili vishindo vya ina akina Wawa.
Makocha wake waliamua kumkimbiza kwanza kwa dakika 90 kabla ya kumpa programu nyingine kwa nia ya kumuandaa vyema kuisaidia Yanga katika mechi zao za Ligi Kuu msimu ujao na zile za kumalizika Kombe la Shirikisho Afrika.
Ipo hivi. Ajibu alikuwa mchezaji pekee aliyeitumikia Yanga msimu uliopita ambaye hakujiunga na timu hiyo sababu zikitajwa kuwa alikuwa mgonjwa lakini akawasili mkoani hapa juzi usiku.
Na jana asubuhi, straika huyo alitua katika mazoezi hayo ambapo ratiba yake ya kwanza alionekana kukimbia pamoja na wenzake wakipasha misuli kwa kuzunguka uwanja mara tatu.
Baada ya zoezi hilo Yanga ikagawanywa katika makundi matatu ambapo makipa walikwenda kwa kocha wao Juma Pondamali.
Kundi la pili likachukuliwa na Kocha Mkuu Mwinyi Zahera likiundwa na nyota wengine wote wa ndani isipokuwa Ajibu, ambaye alikabidhiwa kwa msaidizi wake, Noel Mwandila ambaye kazi yake ya jana ilikuwa ni kumsimamia straika huyo tu.
Mzambia huyo, alianza na kumpa maelekezo mafupi kabla ya mshambuliaji huyo kuanza kukimbia akizunguka uwanja peke yake.
Kila baada ya dakika 30 Mwandila alikuwa akimbadilishia Ajibu programu ya mazoezi kwa kumfanyisha mazoezi ya viungo na mengine ya stamina.
Wakati wote wa mbio hizo wachezaji wenzake wakiwemo Mrisho Ngassa, Kelvin Yondani, Juma Abdul na Emmanuel Martin walionekana kumkejeli wakimwambia mbona kazi bado.
Wachezaji hao walimtaka kuongeza kasi kwa kuwa wao walikutana na dozi kubwa zaidi ya hiyo wakati wakifanya mazoezi mwanzo wa kambi hiyo katika Uwanja wa Jamhuri.
Hata baada ya timu nzima kumaliza mazoezi Ajibu aliendelea na programu hiyo huku makocha waimsubiri katikati ya uwanja.
Kocha Zahera, alisema angependa kuona vijana wake wanakuwa fiti kabla ya kuanza majukumu yao katika msimu mpya wa mashindano, ndio maana aliamua kumkabidhi Ajibu kwa Mwandila adili naye kwa straika huyo alichelewa kambini.
Ajibu alisajiliwa Yanga msimu uliopita akitokea Simba na kuanza kwa makeke kabla ya kupoteza makali mwishoni mwa msimu, akimaliza na mabao saba tu katika Ligi Kuu idadi ambayo ni ndogo kwa msimu mmoja kulinganisha na alivyokuwa Simba aliyoichezea misimu mitatu na kuifungia mabao jumla ya mabao 25 ya ligi.